Full-Width Version (true/false)


Kenya yaanza kuuza mafuta nje ya nchi

 
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya jana june 04, amezindua rasmi usafirishaji wa mafuta ghafi ya petroli yaliyochimbwa nchini humo na kwa utaratibu huo nchi hiyo imeanza mkakati wa kuuza bidhaa hiyo katika soko la kimataifa.

Akiwa katika katika eneo la visima vya mafuta huko Lokichar katika kaunti ya Turkana kaskazini mwa Kenya, Rais Kenyatta amezindua safari za malori manne yatakayosafirisha mapipa 600 ya mafuta hadi katika kiwanda cha kusafisha mafuta kilichoko Changamwe katika Kaunti ya Mombasa. Rais Kenyatta amesema usafirishaji huo wa majaribio ni mwanzo wa safari ndefu itakayozaa matunda.

Mafuta hayo yanatazmiwa kuuzwa katika soko la kimataifa na hivyo kuifanya Kenya iwe miongoni mwa nchi zinazouza mafuta ghafi ya petroli duniani. Rais Kenyatta amesema serikali ya Kenya itajitahidi kuzalisha bidhaa zitokanazo na mafuta ghafi ya petroli ili kuimarisha ustawi na uwekezaji wa kigeni. Aidha amesema Serikali inatekeleza mkakati wa uchimbaji wa gesi nchini humo.

Rais wa Kenya amesema wenyeji wa eneo lenye visima vya mafuta katika kaunti ya Turkana watafaidika na utajiri huo hasa kwa ujenzi wa miundo msingi muhimu.

Mapipa 2,000 ya mafuta yanatarjiwa kusafirishwa kwa barabara kila siku kutoka Turkana hadi Mombasa katika masafa yenye umbali wa kilomita 1,000. Serikali ya Kenya ina mpango wa kujenga bomba la mafuta kutoka eneo la Turkana hadi bandari ya Mombasa kabla ya mwaka 2021 ili kuharakisha usafirishaji wa mafuta hayo katika masoko ya kimataifa.

No comments

Powered by Blogger.