Full-Width Version (true/false)


KOCHA Mfaransa wa Simba, Lechantre ataka mashine nne za kigeni

 

KOCHA Mfaransa wa Simba, Pierre Lechantre hataki masihara kabisa wakati huu akijiandaa na msimu ujao wa mashindano. Lechantre aliyeipa Simba taji la kwanza la Ligi Kuu Bara katika kipindi cha miaka sita iliyopita, amefichua mipango yake ya kukisuka kikosi hicho ili kiwe bora zaidi ambapo sasa anahitaji wachezaji wawili hadi wanne wa kigeni. 

Kocha huyo aliyefundisha soka katika nchi za Tunisia, Algeria pamoja na Uarabuni, alisema kutokana na idadi ya wachezaji saba tu wa kigeni wanaoruhusiwa nchini, aliwaambia mabosi wa Simba wahakikishe wanawasaini wachezaji wote wazuri wazawa ili kujiimarisha zaidi. Simba tayari imewasaini mastraika watatu ambao ni Mohammed Rashid kutoka Prisons ya Mbeya, Marcel Kaheza kutoka Majimaji na Adam Salamba wa Lipuli. 

Lechantre alisema baada ya usajili huo, amependekeza majina ya nyota wengine wanne wa kimataifa kutoka nje ya Tanzania ambao ndio watakamilisha jeshi lake kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi Desemba mwaka huu. 

“Nimewaambia viongozi kuwa kutokana na uchache wa wachezaji wa kigeni, tunahitaji kupata wenye viwango vya juu zaidi. Nimependekeza majina ya wachezaji wanne, tunaweza kuwasajili wawili, watatu ama wote ili kuwa na timu bora. “Kwa sasa nina furaha kwamba tumefanya usajili wa wachezaji wazuri kutoka hapa Tanzania. Tunawahitaji hao kwa kuanzia kutengeneza timu nzuri, tutafanya usajili mwingine mkubwa hapo baadaye,” alisema kocha huyo aliyeipa Cameroon taji la Afrika mwaka 2000. 

ANASEPA 
Katika hatua nyingine, Lechantre alisema hajui hatma yake ya baadaye klabu hapo na anashindwa kuendelea kupanga mipango mingi ndani ya Simba kwani mpaka sasa hafahamu hatma yake na huenda asiwe kocha mkuu wa timu hiyo msimu ujao. Lechantre alisema mpaka sasa hajafikia makubaliano yoyote ya mkataba mpya na Simba, lakini anamsikilizia mfadhali wa timu hiyo, Mohammed Dewji juu ya hatma yake hiyo. “Nimegundua hapa watu wana matarajio makubwa sana. Niliposhinda mechi nyingi walikuwa kimya, tulipofungwa na kutoa sare watu wameumia sana. 

Nahitaji kupewa muda zaidi ili nitengeneze timu mpya. “Mohammed Dewji ana programu nzuri hapa, inahitaji muda. “Ni lazima tukubaliane kwamba kutengeneza timu ya kushinda taji la Afrika inahitajika muda zaidi, nitazungumza naye ili kuona tunafanya nini,” alisema Lechantre. “Mpaka sasa sijafahamu hatma yangu, nashindwa kupangilia vitu vingi hivyo hata hao wachezaji wapya siwezi kusema nitawatumia vipi,” alisisitiza Mfarasna huyo aliyeomba kazi tena Timu ya Taifa ya Cameroon.

No comments

Powered by Blogger.