Full-Width Version (true/false)


Magari yaliotumika kwa zaidi ya miaka 15 marufuku kuingizwa Uganda

 
Magari yaliotumika kwa zaidi ya miaka 15 hayatoruhusiwa nchini Uganda kuanzia Septemba mwaka huu kufuatia kuidhinishwa kwa marekebisho ya mswada wa trafiki na usalama barabarani mwaka 2018.

Watu wengi hununua magari makuu kuu kwasababu ya bei yake nafuu.

Serikali ya Uganda hatahivyo inataka kusitisha magari hayo kuingia nchini ikieleza kuwa sio salama kwa matumizi na huchafua mazingira.Sheria hiyo mpya imenuiwa kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na kusaidia kupunguza ajali barabarani ambazo kwa kiwango kikubwa zimetajwa kutokana na magari ya zamani.

Na huo ni mjadala mkubwa Uganda sambamba na kutafuta jitihada za kupunguza ajali hizo barabarani nchini.

Serikali imetangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kufuatia ajali ya basi iliyosababisha vifo vya watu 20 mwishoni mwa juma.

Utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa Kampala ni mojawapo ya miji inayoshuhudiwa uchafuzi mkubwa wa mazingira Afrika.


Lakini waingizaji magari wanaonya kuwa kupiga marufuku uingizaji wa magari hayo yalio na zaidi ya miaka 15 kutasababisha watu kupoteza ajira na kufanya kuwa vigumu kwa raia maskini Uganda kumiliki magari. 

Mtu hutozwa kodi ya 50% wakati anaponunua gari jipya ambalo kwa kawaida ni ghali. 

Kama njia ya kuwaruhusu Waganda wanunue magari yaliotumika kwa muda mfupi, wabunge wameondosha kodi ya mazingira kwa magari yalio na umri wa chini ya miaka 8.

Mwaka jana raia nchini Uganda waliingiza takriban magari 2,500 yaliotumika nchini kwa mwezi.

Nchi jirani Kenya ilipiga marufuku uingizaji wa magari yaliozidi miaka 8.

Tanzania inaruhusu magari yalo na umri wa kati ya miaka 8 hadi 10 kuingia nchini.


Burundi, Rwanda na Sudan Kusini hazina miaka rasmi ya magari yaliotumika yanayoruhusiwa. 
Rais Yoweri Museveni sasa anahitaji kuusaini mswada huo kuwa sheria kabla uanze kutekelezwa mwanzoni mwa mwezi Julai.

No comments

Powered by Blogger.