Full-Width Version (true/false)


Magereza wakosa gari ya kupeleka mahakamani Aveva, Kaburu


 

Kesi ya kughushi na kutakatisha fedha, inayowakabili vigogo wa klabu ya Simba akiwemo Rais wake, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange imeshindwa kuendelea baada ya Magereza kukosa gari la kuwaleta Mahakamani, washtakiwa hao. 

Hayo yameelezwa leo, Juni 5, 2018 na Wakili wa Takukuru, Leonard Swai, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya uamuzi. Swai alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi, kama mahakama hiyo inauwezo wa kuwaondoa mshtakiwa wa tatu na wanne katika kesi hiyo, ili shauri hilo liendelee kusikizwa kwa washtakiwa waliopo au laa. 

"Kesi hii imekuja kwa ajili ya uamuzi, lakini nimepewa taarifa na Mkuu wa Gereza la Keko, asubuhi hii kuwa wameshindwa kuwaleta washtakiwa Mahakamani hapa, kutokana na kukosa gari la msafara la kuwaleta hapa, hivyo tu naomba tarehe nyingine" alidai Swai. Swai aliendelea kudai kuwa, gari la msafara lililotakiwa kuwaleta washtakiwa hao Mahakamani hapo, limepeleka washtakiwa wengine Mahakama ya Kibaha na Kinondoni

Magereza huwa wana utaratibu wao wa kuwaleta washtakiwa Mahakamani, kuna wanaoletwa kwa msafara mkali na kuna wanaoletwa na msafara wakawaida," alidai Swai. Baada ya Maelezo hayo, Wakili Timotheo Wandiba, anayewatetea Aveva na Kaburu, alieleza mahakama kuwa wapo tayari kusikilizwa uamuzi. 

"Kwa niaba ya wateja wetu, mimi na wenzangu tupo tayari mheshimiwa kusikiliza uamuzi wa mahakama yako" alidai Wakili. Hakimu Simba alisema tayari ameshaanda uamuzi, lakini hataweza kuusoma uamuzi huo wakati washtakiwa hawapo Mahakamani. 

"Siwezi kuwasomea uamuzi wakati washtakiwa hawapo Mahakamani hapa" alisema Hakimu Simba na kuongeza "Kuhusu washtakiwa kushindwa kuletwa Mahakamani hapa, niseme tu sitaki kuingilia mfumo wa ulinzi wa Magereza, wao ndio wanajua na wakati mwingine zinaweza kuwa ni sababu za kiusalama zaidi" alisema Hakimu Simba. Hakimu Simba aliahirisha shauri hilo, hadi Juni 12, Mwaka huu, atakapotoa uamuzi. 

Hatua hiyo ya kutolewa uamuzi unatokana na mawakili wa kina Aveva, Nehemia Nkoko na Timotheo Wandiba, Mei 14, Mwaka huu, kuiomba mahakama itoe amri ya kuwaondo washtakiwa Hanspoppe na Lauwo ambao hawajakamatwa na kubadilisha hati ya mashtaka ili waendelee na usikilizwajiwa wa mashtaka dhidi ya wateja wao ambao tayari wameshasomewa mashtaka. 

Wakili Wandiba alihoji kuwa mahakama itaendelea kuwasubiri washtakiwa hao ambao hajakamatwa Mpaka lini wakati kesi dhidi ya wateja wao ikiwa imesimama? Mbali na Aveva, washtakiwa wengine katika Kesi hiyo ni Zacharia Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba na mfanyabiashara,Franklin Lauwo, ambao mpaka sasa bado hawajakamatwa na juhudi za kuwafatuta ili waunganishwe katika Kesi hiyo zinaendelea.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli. 

Wanadiawa, Machi 10 na 16, 2016, Aveva na Nyange waliandaa nyaraka za kuhamisha dola za kimarekani 3000,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba kwenda kwenye akaunti ya Aveva wakijua kuwa wanachofanya ni kosa. 

Hata hivyo, Aveva na Kaburu, wapo mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria. Itakumbukwa kuwa, April 30, 2018, mahakama hiyo iliamuru washtakiwa Hanspoppe na Lauwo wakamatwe popote walipo. 

Amri hiyo ilitolewa baada ya upande wa mashtaka kupitia kwa Wakili Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai, kuieleza Mahakama hiyo kuwa wamewatafuta washtakiwa hao tangu Machi 16 mwaka huu bila mafanikio.

No comments

Powered by Blogger.