Full-Width Version (true/false)


Magufuli awageukia 'wazinguaji' barabaraniRais Dkt. John Magufuli ameliagiza Jeshi la Polisi hususani Kikosi cha Usalama Barabarani nchini kuwachukulia hatua kali watu wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani kwani wamekuwa wakisababisha kutokea kwa vifo vingi vya wananchi wa kitanzania. 

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anatoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia vifo vya watu 10 vilivyosababishwa na ajali ya basi la abiria kugongana na treni ya mizigo Mjini Kigoma iliyotokea leo Juni 06, 2018 majira ya 12:15 asubuhi. 

"Kwa mara nyingine tumewapoteza watanzania wenzetu 10 katika ajali, tumepoteza wapendwa wetu na tumepoteza nguvu kazi ya Taifa, nawakumbusha wadau wote wa usalama barabarani kuchukua hatua madhubuti za kuzuia ajali hizi, vyombo husika chukueni hatua kali kwa wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani", amesema Rais Magufuli.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli ameendelea kwa kusema "nawapa pole familia na wote mlioguswa na vifo vya ndugu zetu hawa, naungana nanyi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awapumzishe mahali pema peponi, na majeruhi wapate matibabu na wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao” amesema Mhe. Rais Magufuli katika salamu hizo.

Kwa upande mwingine, Dkt. Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brig. Jen. Mstaafu Emanuel Maganga kufikisha salamu hizo kwa wafiwa wote, na amewaombea kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao

No comments

Powered by Blogger.