Full-Width Version (true/false)


Manyika gumzo Kenya wakiifuata Gor Mahia


 
GOLIKIPA Manyika Peter, amekuwa gumzo huko kenya baada ya kiwango chake cha juu alichokionyesha jana na kuisaidia Singida United kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup kwa kuitoa AFC Leopards kwa mikwaju ya penalti 4-2. 

Timu hizo zilifikia hatua hiyo ya penalti baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana huku Manyika akiokoa penalti kwenye kipindi cha pili cha mchezo huo. 

Mapungufu ya mabeki wa Singida United kwenye kipindi cha pili yalifichwa vema na Manyika kwa kuokoa hatari nyingi langoni kwao. 

Mchezaji Elinyesia Sumbi ndiye aliyeipeleka Singida nusu fainali baada ya kufunga penalti ya mwisho iliyowapa ushindi ‘Walima Alizeti’ hao. 

Katika hatua ya matuta, nyota wa Singida aliyetokea Mbeya City, Kenny Ally, alikosa penalti yake ikiwa ni ya kwanza kwa Singida kwenye mchezo huo.

Penalti za Singida zilifungwa na Shafiq Batambuze, Miraji Adam, Danny Lyanga na Sumbi. 

Akizungumzia matokeo hayo, kocha wa Singida, Hemed Morocco, alisema mchezo ulikuwa mgumu hasa kwa upande wao kwa kuwa AFC Leopards ni timu nzuri na walikuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani. 

Alisema anashukuru ni mchezo wake wa kwanza tangu achukue mikoba ya kuifundisha timu hiyo kutoka kwa Hans van der Pluijm, lakini wachezaji wamejitahidi kufuata maelekezo yake. 

“Sasa tunaenda kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao, wapinzani wetu wajao ni wazuri na ndio mabingwa wa Kenya pamoja na michuano hii, tunaenda kujipanga,” alisema Morocco. 

Kwa matokeo hayo, Singida inaungana na Simba kucheza hatua ya nusu fainali baada ya kushuhudia Yanga na JKU ziking’olewa mapema. 

Singida itaumana na Gor Mahia kwenye hatua hiyo keshokutwa saa 9:15 alasiri wakitanguliwa na mchezo wa Simba dhidi ya Kakamega Homeboyz mchezo utakaoanza saa 7:00 mchana. 

Katika michuano hiyo inayoendelea kwenye Uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Kenya, bingwa mbali na kujizolea kitita cha dola za Marekani 30,000, pia atasafiri kwenda kuivaa Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

No comments

Powered by Blogger.