Full-Width Version (true/false)


Mataifa 29 kushiriki maonyesho ya Sabasaba

 
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) imetangaza kuwa nchi 29 zimethibitisha kushiriki maonyesho ya 42 ya kimataifa maarufu Sabasaba yatakayoanza mwishoni mwa mwezi huu. 
 
Mkurugenzi mkuu wa Tantrade, Edwin Rutageruka alisema baadhi ya nchi hizo ni China, Afrika Kusini, Nigeria, Malawi, Japan na Malaysia. Alisema kwamba maonyesho hayo yatafanyika kwa siku 16 kuanzia Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu. 
 
Rutageruka alisema katika maonyesho hayo, kampuni 2,456 za ndani za nchi zimethibitisha kushiriki. Alisema kwamba kampuni za nje zilizothibitisha kushiriki ni 450 lakini zinaweza kuongezeka hadi kufikia 500 kwa sababu bado wanaendelea kuandikisha. 
 
Alisema taasisi za Serikali 120 pia zimethibitisha kushiriki katika maonyesho hayo. Rutageruka alisema asilimia 89.4 ya majengo ya mamlaka hiyo yameshakodishwa na kwamba limebaki jengo moja. “Tunawaomba waliochukua mabanda kwa ajili ya maonyesho kufanya maandalizi mapema. 
 
Haipendezi muda wa maonyesho unaanza ndipo watu wanaanza kupanga bidhaa za maonyesho,” alisema.Mkurugenzi wa huduma wa Tantrade, Martha Paul aliwataka wafanyabiashara wanaotaka maeneo ya kukodi kuwahi vinginevyo watayakosa. 
 
“Kama ilivyoelezwa asilimia 89.4 ya majengo ya Tantrade yameshakodishwa mkiendelea kuchelewa mtayakosa,” alisema.

No comments

Powered by Blogger.