Full-Width Version (true/false)


Mawaziri Wakuu Jordan, Madagascar Wajiuzulu

Mawaziri wakuu Jordan, Madagascar wajiuzulu
Waziri Mkuu Hani al-Mulki amewasilisha barua ya kujiuzulu baada ya kukutana na Mfalme Abdullah II Jumatatu, maofisa wamesema.

Kujiuzulu kwake kumekuja katika kipindi ambacho kumekuwa na maandamano makubwa yaliyochochewa na kupanda kwa bei za vitu na mabadiliko katika sheria ya mapato.

Hatua ya kujiuzulu kwake imelenga kutuliza hasira na ghadhabu za waandamanaji dhidi ya sera za kiuchumi.

Maandamano yamekuwa yakifanyika katika jiji la Amman na miji mingine mikubwa kwa siku nne zilizopita huku waandamanaji wakishinikiza kuondolewa kwa Mulki, ambaye serikali yake ilipendekeza ongezeko la kodi ya mapato kwa asilimia tano.

Mulki aliingia madarakani mwaka 2016 na alikuwa na wajibu wa kuboresha uchumi wa nchi wakati eneo hilo likikumbwa na vurugu na mgogoro wa wahamiaji.

Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika, Waziri wa Elimu Omar al-Razza, anatarajiwa kuteuliwa kuchukua nafasi ya Mulki.

Kutoka jijini Antananarivo, Waziri Mkuu wa Madagascar Olivier Mahafaly amesema amejiuzulu kuanzia Jumatatu ili kutekeleza masharti ya uamuzi wa mahakama iliyoamuru kuundwa kwa serikali ya mpito ili kumaliza mgogoro wa sasa wa kisiasa.

Mwezi uliopita Rais Hery Rajaonarimampianina alipitisha sheria ya mabadiliko ya uchaguzi ambayo inaweza kumruhusu mgombea wa upinzani Marc Ravalomanana kuwania ofisi hiyo.

Toleo la kwanza la sheria hiyo iliibua maandamano mitaani ambayo pia yalisababisha vifo.

Mahakama Kuu ilimwamuru Rajaonarimampianina kuivunja serikali na kumteua wazi mkuu mpya ambaye ataungwa mkono na vyama vyote vya siasa.

Kutoka Yamoussoukro, Ivory Coast. Rais Alassane Ouattara amesema yuko huru kuwania urais kwa muhula wa tatu katika uchaguzi mwaka 2020, chini ya katiba mpya ya nchi hiyo, alisema katika mahojiano yaliyochapishwa kwenye jarida la wiki hii la Ufaransa Jeune Afrique.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ouattara aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2010, katika uchaguzi uliosababisha machafuko ya muda mfupi katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, kutoa kauli hiyo ambayo itawaghadhabisha mahasimu wake kisiasa.

“Katiba mpya inaniruhusu kuongoza mihula miwili kuanzia mwaka 2020,” Ouattara mwenye umri wa miaka 76 aliliambia Jeune Afrique ikiwa na maana mihula miwili aliyoongoza chini ya katiba ya zamani haitahesabika bali katiba mpya inayotaja ukomo kuwa mihula miwili.

“Nitatoa uamuzi wangu wa miwsho wakati huo kwa kuangalia hali ilivyo ya kisiasa nchini Ivory Coast. Utulivu na amani ndiyo kipaumbele kabla ya yote ikiwemo misingi imara,” alisema.

Msemaji wa serikali hakupatikana kutoa ufafanuzi kuhusu maendeleo haya mapya ya kisiasa. Awali Ouattara aliahidi kung’atuka ifikapo 2020.

No comments

Powered by Blogger.