Full-Width Version (true/false)


Mrithi wa Jecha anukia

 

BAADA ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha pamoja na wajumbe wa tume hiyo kumaliza muda wao wa uongozi, mrithi wa Jecha anatarajiwa kutangazwa hivi karibuni. 

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, juzi alikutana na viongozi wa vyama 17 vya siasa Ikulu mjini Zanzibar, ili kushauriana namna bora zaidi ya kuwapata wajumbe wawili watakaoteuliwa katika ZEC kutoka vyama vya upinzani. 

Miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa waliohudhuria kikao hicho ni Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa, Prof. Ibrahim Lipumba. Hatua hiyo imekuja kwa ajili ya kutekeleza maelekezo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 juu ya kuwapata wajumbe wa ZEC. 

Aidha, mkutano huo umefanyika baada ya ZEC kumaliza muda wake chini ya Mwenyekiti Jecha. Tume hiyo ilitekeleza majukumu yake kwa miaka mitano kuanzia Aprili, 30, 2013 mpaka Aprili 29, 2018. 

Kifungu namba 119 (1) c cha Katiba ya Zanzibar, kinaeleza kuwa wajumbe wawili watateuliwa na Rais kwa mapendekezo ya Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi au kushauriana na vyama vya siasa iwapo hakuna kiongozi wa upinzani. 

Dk. Shein aliwataka viongozi hao watakapomaliza taratibu za kuwapata wateule wao wampe majina, ili ayateue kupitia (ZEC) atakayoitangaza hivi karibuni. 

Alisema ameona haja ya  kuwaita viongozi hao wa vyama vya siasa ili kushauriana nao juu ya nafasi hizo kutokana na hivi sasa kutokuwapo kwa kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. 

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa nia yake ya kufanya hivyo ni kujenga Zanzibar kwa umoja na mshikamano na kuahidi kuwa hatobeza mawazo ya vyama vya siasa vya upinzani na kuahidi kutenda haki katika kuchagua viongozi wazuri. 

Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo ndio njia pekee itakayosaidia zaidi kuimarisha uongozi wa demokrasia hapa nchini huku akitumia fursa hiyo kuyapongeza mawazo ya viongozi hao wa vyama vya siasa waliyoyatoa katika kikao hicho. 

Nao viongozi hao waliohudhuria waliupongeza uamuzi wa Dk. Shein wa kuwaita kwa lengo la kushauriana nao pamoja na kueleza kuwa kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa kiongozi huyo amebobea katika demokrasia na utawala bora. Viongozi hao walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kuvishirikisha vyama vya siasa na kumpongeza kwa jinsi anavyoongoza nchi kwa hekima na busara.

No comments

Powered by Blogger.