Full-Width Version (true/false)


Mwanza: 35 mbaroni kwa kujichukulia sheria mikononi


Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu 35 kwa tuhuma za kuchoma moto gari lililowagonga watoto wawili wa familia moja na kusababisha kifo cha mmoja wao katika barabara ya Igombe eneo la Kayenze ndogo wilayani Ilemela majira ya asubuhi  juni 7 mwaka huu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa polisi Ahmed Msangi amemtaja mwanafunzi aliyefariki papo hapo kuwa ni Naomi Opio mwenye umri wa miaka 12 mwanafuzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Kisundi, huku mdogo wake aitwaye Baton Opio mwenye umri wa miaka 9 anayesoma darasa la tatu katika shule hiyo akijeruhiwa kichwani na kuvunjika mkono wa kulia na amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou toure kwa matibabu zaidi.

kamanda Msangi ameongeza kuwa katika tukio hilo wananchi hao pia wanadaiwa kumvamia na kumjeruhi dereva wa magari ya kwenda Igombe aliyefahamika kwa jina la Azizi Mohamed kwa kumpiga mawe na kumchoma na vitu vyenye ncha kali sehemu za mgongoni baada ya kuwasihi kuacha kujichukulia sheria mkononi kitendo ambacho ni kinyume cha sharia.

Kutokana na tukio hilo Kamanda wa polisi mkoani humo Ahmed Msangi ameitaka jamii kujiepusha na matukio ya uvunjifu wa amani na kujichukulia sheria mkononi huku akiwasihi madereva kuwa waangalifu wawapo barabarani.

No comments

Powered by Blogger.