Full-Width Version (true/false)


Obama kutua tena Kenya mwezi ujao
Barack Obama atafanya ziara ya siku moja nchini Kenya Julai 16. Akiwa nchini humo, Obama atakutana na kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi na baadaye ataelekea katika kijiji cha wazazi wake cha K’Ogelo. Kwa mujibu wa gazeti na Daily Nation baada ya hapo Obama ataelekea Afrika Kusini ambako anatarajiwa kutoa mhadhara katika kongamano la kila mwaka la Nelson Mandela. 

Katika ziara hiyo Obama hataambatana na familia yake. Itakuwa ni mara yake ya kwanza kuzuru nchini humo tangu aondoke madarakani Januari 20 mwaka jana. 

Mara tatu alizotembelea Kenya ni pamoja na mwaka 1987, 1992 na mwaka 2015 wakati akimalizia muhula wake wa mwisho wa uongozi. Katika ziara yake ya mwisho nchini pia hakuwa ameambatana na familia yake. Taarifa zaidi zinasema kuwa akiwa nchini humo Obama ambaye bado anaendelea kukubalika nchini Marekani huenda akakutana pia na viongozi wa vyama vya upinzani. 

“Ziara yake imekuwa ikichambuliwa kwa muda wa wiki mbili sasa. Bado ni mapema mno kujua mengi lakini atawasili Kenya wakati akiwa safarini kuelekea Afrika Kusini,” chanzo kimoja cha habari kilidokeza.

Ikulu haijathibitisha chochote kuhusiana na ziara hiyo na alipotafutwa msemaji wake, Manoah Esipisu alielekeza wahusika wawasiliane na ofisi ya Obama kupata taarifa zaidi.; “Ofisa ya Obama ndiyo itakayotangaza,” alisema Manoah alipoombwa kutoa ufafanuzi kuhusu ziara hiyo. 

Duru za habari zinaeleza kuwa kampuni moja inayosifika kwa shughuli za mawasiliano kwa umma tayari imekodiwa kusaidia uratibu wa ziara hiyo. Ubalozi wa Marekani mjini Nairobi uliahidi kuwa leo ungetoa majibu kuhusiana na ziara hiyo. 

Ofisa habari ubalozini hapo, Jim Onyango alipotafutwa na gazeti la Daily Nation alitaka atumiwe maswali kwa njia ya kiofisi. Tunapendelea mtuletee barua rasmi kwa njia ya baruapepe nasi tutajibu Jumatatu,” alisema.

No comments

Powered by Blogger.