Full-Width Version (true/false)


Onyo wanaodanganya passport

 


WANANCHI wasio raia wa Tanzania wameonywa kutojitokeza kufanya udanganyifu, ili wapatiwe hati za kusafiria na kuwa watakaojaribu kufanya hivyo na kubainika watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

Onyo hilo lilitolewa na Kamishna wa Uhamiaji wa Uraia na Hati za Kusafiria, Gerald Kihinga, wakati wa uzinduzi rasmi wa hati za kielektroniki, uliofanyika katika Manispaa ya Bukoba mwishoni mwa wiki. 

Kihinga alisema kuwa ili mwananchi aweze kupewa hati hizo mpya, moja ya kigezo ni kuwa na kitambulisho cha taifa, lakini sio kwamba kila mwenye kitambulisho hicho ndio sifa ya kuwa ni Mtanzania. 

“Inawezekana kuna watu wanajipenyeza na kupatiwa kitambulisho cha taifa wakati sio Watanzania, inabidi watambue kuwa watakapokuja kupatiwa hati hizi, mhusika anatakiwa pia kuwasilisha nyaraka nyingine, kwa hiyo atakayejaribu kujipenyeza atakamatwa," alisema. 

 Kihinga alisema kuwa Uhamiaji watafanya kila linalowezekana, ili kuhakikisha hati hizo za kielektroniki haziangukii mikononi mwa wasio raia, maana zinatolewa kwa ajili ya Watanzania. 

Alisema tangu Rais John Magufuli azindue mradi wa Uhamiaji mtandao Januari 31 mwaka huu, wamekwishafunga mifumo ya kutoa hati hizo katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, na sasa Kagera. 

"Tunatarajia ifikapo mwishoni mwa Julai mwaka huu, tutakamilisha kufunga mifumo hii nchi nzima, na tangu mradi ulipozinduliwa hadi Juni 07 mwaka huu, tumekwishatoa hati za kielektroniki 17,598," alisema Kihinga. 

Akizindua rasmi zoezi hilo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo, alisema kuwa pamoja na mambo mengine mfumo wa Uhamiaji mtandao unalenga kukidhi matakwa ya usalama wa nchi. 

Kinawilo alisema kuwa wapo baadhi ya watu walitumia vibaya hati za kusafiria za zamani na kuleta sifa mbaya kwa taifa, na kuwa hati hizo mpya zina uwezo wa kukabiliana na changamoto hiyo. 

Alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la utoaji wa kitambulisho cha taifa linaloendelea mkoani Kagera, maana kitambulisho hicho ni moja ya sifa wakati wa kuomba hati hizo. 

Naye ofisa wa Uhamiaji mkoa wa Kagera, Abdallah Towo, alisema askari wote wa idara hiyo wamepewa elimu ya namna ya kuwahudumia raia na kuwa anategemea wananchi watapewa huduma inayostahili. 

"Watu wote watahudumiwa kwa utaratibu ule ule, ikionekana kuna mtu kahudumiwa tofauti na wengine na kusababisha kuwepo na shaka, tunaomba kupatiwa taarifa za haraka ili hatua zichukuliwe," alisema Towo. Mkoa wa Kagera unahofiwa kuwa na watu wengi wasio raia wa Tanzania, kutokana na kupakana na nchi nyingi, zikiwamo Rwanda, Burundi na Uganda.

No comments

Powered by Blogger.