Full-Width Version (true/false)


Orodha wabunge wadaiwa sugu yawekwa wazi

 

SPIKA wa Bunge Job Ndugai amekiri kupokea orodha ya wabunge wanaodaiwa fedha za matrekta na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) kwa muda mrefu. Aidha, Spika Ndugai amesema ameshindwa kuwakata madeni hayo juu kwa juu wabunge hao kutokana na baadhi yao kuwa hawana fedha ya ziada. 

Akitoa tangazo la madai hayo bungeni jana, Ndugai alisema Mei 17, mwaka huu Rais John Magufuli aliagiza wadaiwa sugu wa Suma JKT walipe madeni yao. “Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imewasilisha orodha ofisi ya Spika ya wadaiwa wa fedha za matrekta na (wabunge husika) mnatakiwa kulipa madeni haya haraka iwezekanavyo,” alisema. 

Alisema wabunge hao waliokopa matrekta na vipuli vyake, wanatakiwa kulipa kabla ya Juni 23 - ndani ya siku 18. “Nina orodha ndefu hapa sijui niisome?" Alisema Ndugai, na kwamba "kuna wengine nimejaribu kuangalia basi hata wakatwe juu kwa juu kwenye fedha hizi tunazopata pata, lakini hawana hata fedha kabisa. 

Sina pa kukata, sasa kwa kweli jitahidini tu.” Mei 17, katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Uwekezaji cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo, alimweleza Rais Magufuli kuwa JWTZ linaidai sekta binafsi Sh. bilioni 40, huku taasisi za serikali zikidaiwa Sh. bilioni 3.4, jambo ambalo limekuwa likiwakwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo. 

Ili kuliwezesha jeshi hilo kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo, Jenerali Mabeyo alimuomba Rais apokee orodha ya wadaiwa ili aongeze msukumo katika ulipaji wake. Kufuatia ombi hilo, Rais Magufuli alitoa muda wa mwezi mmoja kwa wadaiwa wote kuhakikisha wamelipa madeni wanayodaiwa na kuagiza baada ya kuisha kwa kipindi hicho, mamlaka zinazohusika na ukusanyaji wa madeni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua kali wadaiwa wote. 

ZITTO ALIANIKA
Desemba 30, 2016 Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alianika kiwango cha mshahara wa Mbunge na aina ya malipo ya posho wanazopata wanapokuwa kwenye utumushi wa miaka mitano. Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook alidai mshahara wa mbunge kwa mwezi ni Sh. milioni 4.6 kabla ya kodi. Alisema baada ya kukatwa kodi ya mapato, Mbunge hubakia na Sh. milioni 3.2 kwa mwezi, hivyo kufanya mshahara wa Sh. milioni 38.4 kwa mwaka. 

Zitto alidai pia Mbunge hulipwa Sh. milioni 8.2 kila mwezi kama posho ya kazi za Ubunge ambazo ni kwa ajili ya mafuta ya kutembelea Jimbo, matengenezo ya gari, malipo ya watumishi wa Ofisi ya Mbunge kama vile dereva, mhudumu wa ofisi na katibu wa Mbunge. 

"Hii ndio inapelekea mapato ya jumla ya Sh. milioni 99 kwa mwaka niliyoweka kwenye taarifa ya rasilimali na madeni," aliandika Zitto. Mbunge pia hulipwa posho za kujikimu na posho za vikao ambazo hutolewa kulingana na mahudhurio ya vikao.

No comments

Powered by Blogger.