Full-Width Version (true/false)


Paul Makonda apiga marufuku uvaaji wa sketi fupi "vimini" Dar

 


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametaka kinadada wanaovaa nguo fupi na za kubana kuziacha katika mwezi huu wa Ramadhani ili kina baba Waislamu waendeleze funga zao vizuri. 

Makonda aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akipokea kontena moja la tende kutoka Taasisi ya Darul Irshaid Islamic Center, kama sehemu ya sadaka kwa Waislamu katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. 

“Kinadada wanaopenda kuvaa nguo fupi na za kubana, mwezi huu wa Ramadhani tuwaache kina baba hawa watekeleze funga yao vizuri," alisema Makonda. "Na kama unaona huna nyingine, nunua tu dera, livae, pita barabarani ili uache amani. "Usiharibu funga za watu.” Aidha, Makonda alisema tende hizo zitakwenda kwa watoto yatima walioko ndani ya mkoa wake amabao nao wamejitoa kushiriki katika ibada hiyo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. 

Alisema ni vyema nao wakafikiwa na msaada huo ili funga yao na futari yao ikawe na tija kama vitabu vya dini vinavyohimiza kusaidia makundi mbalimbali katika jamii. 

Makonda pia aliwataka wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam; hasa wale ambao hawako katika mfungo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Waislamu ambao wako katika mfungo ili kuhakikisha bei za vyakula haziendelei kupanda kama sehemu ya kujichumia faida bali kuungana nao kama sehemu ya ibada. 

“Tusitumie imani ya Kiislamu kupandisha bidhaa kwa kuwakomoa kwasababu wao ni lazima watimize imani yao," alisema Makonda ambaye alisema upandishaji holela wa bei utafanya "funga yao kuwa ngumu.” Kwa upande wake, mwenyekiti wa taasisi ya Miraji Islamic, Arif Abdulrahman alisema wameamua kutoa tende hizo kama sehemu ya sadaka katika mwezi wa Ramadhani. 

Abdulrahman alisema misaada hiyo inatokana na wageni wengi ambao wanakuja kutembelea misikiti na madrasa nchini na katika ziara zao huguswa na shida za wananchi na hivyo wanaporejea makwao huleta misaada zaidi ili kuwafikia walengwa.

No comments

Powered by Blogger.