Rwanda yapitisha sheria mpya kupambana na uhalifu wa mtandaoni

Bunge nchini Rwanda, Alhamisi
lilipitisha sheria ya uhalifu wa mtandaoni yenye nia ya kuisaidia sekta
za kiserikali na binafsi kudhibiti uhalifu huo.
Bunge la juu
lilipitisha muswada na kupeleka kwenye bunge dogo. Bado muswada
unahitaji kupitishwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame kabla ya kuanza
kufanya kazi.
Sheria inalenga kulinda taarifa za serikali na
binafsi na miundombinu dhidi ya uhalifu wa mitandaoni na mashambulizi ya
mitandaoni, kwa mujibu wa Wizara ya habari na mawasiliano na Teknolojia
ya Rwanda.
''kwa sasa tunashuhudia mashambulizi ya mitandaoni
duniani kote. Mashambulizi ambayo yanatishia usalama wa uchumi na
usalama wa taifa,'' alieleza Agnes Mukazibera, Rais wa Bunge la Rwanda,
baada ya kura.
Sheria itaisaidia serikali kufanya uchunguzi vitisho vyovyote na
kushtaki dhidi ya vitendo hivyo katika taasisi binafsi na za umma na
kuitetea nchi dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni.
Mwaka 2016 Rwanda ilidhibiti zaidi ya mashambulizi ya
mitandaoni 1,000 kila siku kabla ya kuleta madhara kwa
walengwa,makampuni na taasisi,kwa mujibu wa Benki kuu Rwanda.
Mwaka
huo huo, Rwanda ilizindua mfumo wa usalama wa mtandao uliogharimu dola
za kimarekani milioni tatu kwa ajili ya kulinda taasisi binafsi na za
serikali dhidi ya uhalifu wa mitandaoni.
Kwa mujibu wa utafiti,
Kenya ni nchi inayoshambuliwa zaidi na wahalifu wa mitandaoni katika
eneo la Afrika Mashariki, huku biashara nchini humo zikipoteza kiasi
cha dola milioni 146 kutokana na uhalifu wa mitandaoni.
Rwanda inakuwa nchi nyingine katika Afrika mashariki kuidhinisha sheria zinazolenga uhalifu katika mitandao.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliidhinisha mswada wa Uhalifu wa Kompyuta na Mtandaoni wa 2018 kuwa Sheria, hatua itakayotoa adhabu kali kwa watakaopatikana na makosa ya mtandaoni.
Sheria
hiyo inatoa adhabu ya faini ya Sh5 milioni (dola 50,000 za Marekani) au
kifungo cha miaka miwili jela, au adhabu zote mbili, kwa
atakayepatikana na kosa la uenezaji wa habari za uzushi.
Sheria mpya Kenya ya kupambana na uhalifu katika
mtandao inafuata nyingine kama hiyo katika mataifa ya Afrika Mashariki
kuwaadhibu watu wanaosambaza 'habari za uongo'na kutoa adhabu kali kwa
wahalifu wa mitandaoni.
Hali sio tofuati sana katika nchi jirani
ya Tanzania ambapo maafisa hivi maajuzi walitangaza sheria mpya
zinazowahitaji wanablogu kulipa .
Serikali inasema inataka
kulilinda taifa hilo dhidi ya 'uongo' unaosambazwa katika mitandao,
licha ya kwamba wakosoaji wanaiona hatua hiyo kama njia ya kukandamiza
uhuru wa kujieleza.
Rais John Magufuli amesema ananuia kukabiliana na anachokitaja kuwa ni 'ugonjwa'.
Hatahivyo mahakama kuu nchini ilizuia utekelezaji wa
sheria hiyo mnamo Mei 5 baada ya kundi la wanaharakati na wawakilishi
kutoka vyombo vya habari nchini kuzusha pingamizi.
Iwapo sheria
hiyo itapita kesi iliyopo kotini, inatoa adhabu ya faini isiyo chini ya
$2,000 au kifungo kisicho chini ya mwaka mmoja au yote mawili kwa
wahalifu watakaopatikana na makosa.
Nchini Uganda, serikali ya rais Yoweri Museveni imezuia mipango
ya kuidhinisha kodi ya kutumia mitandao ya kijamii baada ya wizara ya
fedha kusema inahitaji kushauriana kuhusu vipi mpango huo wa kodi
utaweza kuidhinishwa.
Museveni alipendekeza watu watozwe kodi kwa kutumia
mitandao ya kijamii Facebook na WhatsApp, akisema kodi itakayokusanywa
italisaidia taifa hilo kukabiliana na athari za Olugambo [uvumi]".
Wakosaji
wanasema nia ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 73 ni kukandamiza
vyombo vya habari na wale wanaopinga mpango wake wa kuwania tena urais
katika uchaguzi mkuu wa 2021.
Serikali yake ilifunga mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi mkuu mnamo 2016
No comments