Full-Width Version (true/false)


Sababu tano zilizoiponza Yanga iondolwe mapema michuano ya sportpesa

 

Kabla ya swala ya Alasiri. Kabla ya jogoo wa mchana kuwika. Kabla watoto hawajarudi kutoka mashuleni, habari ya Yanga ilikuwa imemalizika hapa Nakuru. 

Inatia huruma sana. Yanga yenye historia kubwa na soka la Afrika Mashariki. Yanga iliyoshinda mataji matatu ya Ligi Kuu katika miaka minne iliyopita ilikuwa inatia huruma mjini hapa. Imefungwa na timu dhaifu kutoka Kenya. Ni Kakamega Homeboys ambayo kwa sasa inashika nafasi ya tisa kwenye Ligi Kuu ya Kenya. Inashangaza sana. 

Ni utoto ulioje. Yanga haikuwa timu ya kufungwa na Homeboys. Kabla ya mchezo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini uwanjani ilikuwa ovyo. Hadi mechi inamalizika, Yanga ilikuwa imechapwa mabao 3-1. Aibu iliyoje. Mwanaspoti ambayo imeweka kambi mjini hapa, inakuletea sababu tano zilizoiponza Yanga kwenye mchezo huo. 

Upangaji wa kikosi 
Yanga ilianza kupotea mapema tu kwenye mchezo dhidi ya Kakamega Homeboys. Ilipanga kikosi cha ajabu. Winga zake mbili zilikuwa na Baruan Akilimali na Juma Mahadhi. 

Wachezaji ambao msimu uliopita walikuwa ovyo. Yanga ilicheza na kiungo mmoja tu halisi wa kukaba, alikuwa Papy Tshishimbi. Mbele yake alicheza Pius Buswita na Edward Maka. 

Hawakuwa na kiwango cha juu. Matokeo yake Yanga ilizidiwa katika dakika 30 zote za mwanzo. Beki yake ya kati pia ilipwaya chini ya Said Juma ‘Makapu’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’. Matokeo yake katika dakika 30 tu za mwanzo, Yanga ilikuwa nyuma kwa mabao mawili. 

Mabadiliko ya ajabu Yanga ilizidiwa kwenye safu ya kiungo tangu mwanzo wa mchezo. Kakamega walicheza kwa kadri walivyojisikia. Walipiga pasi kama vile wanacheza na timu fulani dhaifu kutoka Tanzania. Ajabu ni kwamba Raphael Daudi na Thaban Kamusoko walikuwa kwenye benchi kwa muda wote. 

Ilitarajiwa kocha angepunguza winga mmoja na kuongeza kiungo, lakini hakufanya hivyo.Mabadiliko ya Baruan Akilimali ambayo yalipaswa kumpa nafasi Raphael au Kamusoko, yalishuhudia akiingia Amissi Tambwe. Mchezaji kutoka majeruhi. 

Mchezaji ambaye hana utimamu wa kutosha wa mechi. Tambwe angeisaidia nini Yanga kwa wakati huo? Baadaye wakati mechi imewakalia mkao, wakamtoa Matteo Antony ambaye mbali na kufunga bao la kwanza, alikuwa pia msumbufu kwa wapinzani wao. 

Ilishangaza sana. Utoto mwingi Pamoja na kufungwa mabao ya mapema. Pamoja na kuonekana kuwa ikitokea wameweka uzembe kidogo tu, watapoteza mchezo. Yanga haikuweza kucheza kwa kiwango cha juu. Wachezaji wake walikuwa ovyo muda mwingi uwanjani.

Tshishimbi alikuwa ovyo. Makapu na Tambwe pia walikuwa ovyo. Ni wachezaji wachache tu waliokuwa kwenye kiwango bora. 

Hassan Kessy alijitahidi lakini bado alikuwa na makosa mengi. Kukosekana kwa mastaa Ikumbukwe kuwa kwenye mechi dhidi ya Kakamega Yanga ililazimika kucheza bila ya wachezaji wake watatu wa kikosi cha kwanza. 

Ni Kelvin Yondani, Andrew Vincent ‘Dante’ na Obrey Chirwa. Hawa ni wachezaji muhimu. Kukosekana kwa Dante na Yondani kuliifanya safu ya ulinzi ya Yanga iwe ovyo. Kuliifanya Yanga ishindwe kujiweka salama. Hata penalti iliyopatikana ilitokana na kukosa uzoefu kwa Ninja na Makapu. 

Yondani ndiye roho ya ulinzi ya Yanga kwa sasa. Chirwa ndiye mpachika mabao wao. Amefunga mabao zaidi ya 30 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Kukosekana kwake kuliifanya Yanga imtegemee Matteo Antony ambaye hata hivyo baadaye yalifanyika maamuzi ya kijinga kumtoa. Uchovu wa mashindano Huenda ikawa sababu ya kipuuzi lakini nayo ilichangia Yanga kufungwa kizembe na Homeboys. 

Wachezaji wa Yanga wamechoka Mashindano mbalimbali waliyoshiriki msimu uliopita yamewaacha hoi. 

Yanga ilishiriki Ligi Kuu, Kombe la Mapinduzi, Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho na sasa SportPesa Super Cup. Wachezaji lazima wachoke, hasa ikizingatiwa kuwa wanaocheza ni wale wale. Wachezaji karibu wote wa Yanga wako hoi. Wakipoteza mpira hawawezi kukaba kwa kasi. Wakipata mpira hawawezi kushambulia kwa kasi. Wanastahili mapumziko

No comments

Powered by Blogger.