Full-Width Version (true/false)


Serikali:kuyumba kwa Yanga kumepunguza msisimuko wa soka nchini

 


Serikali imekiri kuwa kutetereka kwa klabu ya soka ya Yanga kumepunguza msisimko wa soka nchini, hivyo kutoa siku 60 kufanya uchaguzi ili kuziba nafasi zilizo wazi. 

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, wakati akifungua mkutano mkuu wa klabu ya Yanga uliofanyika katika Ukumbi wa Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam. 

Alisema hadhi ya Yanga ni kubwa kutokana na kuchukua ubingwa mara nyingi kuliko timu nyingine hapa nchini, hivyo haistahili kupitia hali iliyopo sasa. “Kuterereka kwa Yanga kunagusa wengi ndani na nje ya Bara la Afrika, ndio maana Serikali inaingilia kati kuinusuru klabu hii kwa kuwataka wanachama watambue thamani ya Yanga kuwa ni kubwa,”alisema Dk. Mwakyembe. 

Aidha, Mwakyembe alieleza kuwa ili Yanga ikae sawa inatakiwa kufanya uchaguzi na kuziba nafasi zilizo wazi ndani ya miezi miwili, wakati ikiendelea na mchakato mwingine wa kutafuta mwekezaji. 

“Kaeni mjitathmini upya na mchague watu wenye tija ambao wataleta maendeleo ndani ya klabu hii kongwe, najua kuna maadui wengi pembeni ambao hawapendi kuona mnapata mafanikio. 

“Hata jana kuna watu waliandika barua ofisini kwangu wakitaka mkutano huu usitishwe, lakini nilichowajibu kwa kuwa ni wanachama nimewaambia walete hoja zao mezani zijadiliwe kwa pamoja, Wanayanga wana fursa kubwa hivyo kinachotakiwa ni kubadili mwenendo wao. 

“Bila Yanga imara usajili utakuwa mbaya, timu itafungwa na mapato yatashuka, mfano mechi dhidi ya Mwadui mapato yaliyopatikana ni shilingi laki sita na timu ikapata mgawo wa shilingi laki moja, endapo hali hii itaendelea mapato yatashuka zaidi,” alisema. 

Alisema katika kudhihirisha kuwa Yanga ni klabu kubwa barani Afrika, imependekezwa kuwa kumbukumbu ya bara hilo kutokana na harakati zake za ukombozi ikitumia zaidi michezo na vijana. 

Aidha, Dk. Mwakyembe alisisitiza kuwa katika kipindi hiki cha mpito, viongozi wanatakiwa kukaa na wale wapenzi wa timu wenye uwezo kifedha ili kusaidia kusukuma gurudumu hilo wakati wakiendelea na mchakato wa uwekezaji.

No comments

Powered by Blogger.