Full-Width Version (true/false)


Sikukuu ya Idd kufanyika Dar kitaifa

 

BARAZA Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), limetangaza kuwa swala ya Idd- El- Fitir kitaifa mwaka huu itafanyika jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema swala hiyo ya Idd El Fitr inatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa Juni 15 au 16 mwaka huu katika viwanja vya Mnazi Mmoja. 

Alisema swala hiyo itafanyika kuanzia saa 1:30 asubuhi na kufuatiwa na Baraza la Idd, saa 9:00 Alasiri, litafanyika hapo hapo viwanja vya Mnazi Mmoja na mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli. 

Alhad Mussa alisema Waislam wote wanaalikwa kushiriki katika sherehe hizo za Baraza la Idd zitakazojumuisha burudani za kawaida toka vikundi vya Firqatus Salam, Daarul Maarifa Tenzi na mashairi mbalimbali kuanzia saa 9:00 Alasiri hadi saa 12:00 jioni “Miongoni mwa viongozi tutakaoswali nao ni Rais wa Awamu ya Pili, Alli Hassan Mwinyi, viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, serikali na waheshimiwa mabalozi wa nchimbalimbali,” alisema. 

Aidha, Alhad Mussa aliwatahadharisha Waislam kusherehekea siku hiyo bila maasi ya namna yoyote ile kwa sababu kumuasi Mungu katika siku ya Idd ni sawa na kumuasi katika siku ya kiama. 

Pia aliwataka Waislam na Watanzania wote kwa ujumla, wazidishe mshikamano, amani na umoja hususani katika kipindi hiki cha sikukuu.

No comments

Powered by Blogger.