Full-Width Version (true/false)


Simba izingatie ushauri wa Magufuli mapema


 

MICHUANO ya Kombe la SportPesa Super Cup imemalizika jana kwa mabingwa watetezi, Gor Mahia kutwaa tena ubingwa huo kwa kuichapa Simba kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya fainali iliyopigwa katika Uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Kenya. 

Katika mechi hiyo, Simba ambao ni mabingwa wa Tanzania Bara, walizidiwa kila idara licha ya kuwa na nyota wao wapya waliowasajili kwa ajili ya Ligi Kuu msimu ujao sambamba na michuano ya kimataifa. Ikumbukwe mwakani Simba itakuwa na jukumu la kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika wa 2017/18. 

Simba ambayo katika michuano hiyo haikuwa na washambuliaji wake hatari, Mganda Emmanuel Okwi na Mtanzania John Bocco, hadi michuano hiyo inamalizika haikufanikiwa kupata bao hata moja ndani ya dakika 90. 

 Mechi ya kwanza Simba iliibuka na ushindi wa penalti 3-2 dhidi ya Kariobangi Sharks baada ya matokeo tasa ya dakika 90 za mchezo, huku ya nusu fainali ikishinda tena kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya Kakamega Homeboyz baada ya matokeo tasa tena. 

Matokeo hayo yamefichua mapema tatizo la safu ya ushambuliaji, na ni wazi Simba inahitaji kufanya mapinduzi makubwa ya usajili ili kuweza kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa hapo mwakani. 

Wengi walitarajia kuona uwezo mkubwa ukionyeshwa na washambuliaji Adam Salamba, Marcel Kaheza na Rashid Juma waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao, lakini kwa kiwango walichoonyesha kimedhihirisha wazi Simba inafanya usajili usio makini na kutozingatia michuano inayowakabili. 

Ingawa Simba inaweza kudai kushindwa kufanya vizuri katika michuano hiyo ni kutokana na kuwakosa washambuliaji wake hatari, Okwi na Bocco, kamwe Nipashe hatuwezi kukubaliana na madai kama hayo. 

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba tunaamini, ipo siku itatokea ikiwa katika michuano ya kimataifa kujikuta Okwi na Bocco wote ni majeruhi ama wana matatizo mengine kama ya kifamilia ambayo yanaweza kusababisha kukosekana dimbani jambo ambalo italifanya kukosa mbadala sahihi wa straika anayeweza kubadili matokeo dimbani. 

Kwa mantiki hiyo, Simba inapaswa kutazama vema sera zake za usajili kwani kwa mtiririko wa usajili inaoufanya ni wazi kabisa haiwezi kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alivyosema wakati alipoalikwa kuikabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu na kushuhudia mechi kati ya timu hiyo na Kagera Sugar. 

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu, Kagera Sugar ilionyesha soka safi na kushinda kwa bao 1-0, jambo ambalo Magufuli alisema wazi kwa mpira Simba iliouonyesha haiwezi kufika mbali kimataifa. Hivyo, kutimia kwa kauli hiyo ya Magufuli mapema, hakuna budi kuchukuliwa kama changamoto kwa Simba kumulika upya aina ya usajili wanaoufanya katika kipindi hiki dirisha la usajili likiwa wazi. 

Kinachoonekana kwa Simba ni kufanya usajili wa kuikomoa Yanga, kwa kuwahi wachezaji klabu hiyo ya Jangwani inaotaka kuwasajili, jambo ambalo haliwezi kuisaidia timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam kuelekea katika michuano ya kimataifa hapo mwakani. 

Nipashe tunalazimika kutoa ushauri huo mapema hasa tukizingatia kuwa Gor Mahia ni moja kati ya timu nyepesi ukilinganisha na miamba ya Afrika ambayo Simba inaweza kukutana nayo kwenye michuano ya kimataifa mwakani. 

Hivyo, kwa kushindwa kufurukuta dhidi ya timu hiyo ya Kenya, Simba isitarajie muujiza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama haitabadilika kwa kumulika upya aina ya usajili inayofanya kulingana na michuano inayowakabili.

No comments

Powered by Blogger.