Full-Width Version (true/false)


Simba 'wakoro' wahamishiwa Selous

 

SIMBA sita wakorofi wamehamishwa kutoka Hifadhi ya Wanyamapori Burunge kwenda Pori la Akiba la Selous, baada ya kuonekana kuwa tishio kwa maisha ya binadamu na mifugo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Hamis Iddi Malinga, alisema hayo wakati akisoma taarifa fupi ya halmashauri yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, ambaye anafanya ziara ya siku nne katika halmashauri hiyo. 

Alisema simba hao walihamishwa hapo hivi karibuni. 

Alisema uhamishaji wa wanyama hao ulifanywa kwa ushirikiano na halmashauri, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Nchini, (Tawiri) na taasisi inayoshughulika na utafiti wa simba katika mfumo wa ikolojia wa Tarangire-Ziwa Manyara pamoja na Taasisi ya Uhifadhi ya Chemchem. 

Alisema taasisi hizo zilifanya tathmini ya simba ambao walikuwa tishio kwa maisha ya binadamu na mifugo katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge na hivyo kufanikiwa kuhamishasimba hao sita waliopelekwa Pori la Akiba la Selous. 

Alisema halmashauri yake inasimamia maeneo yenye mtawanyiko wa wanyamapori ambayo yanazunguka Hifadhi za Taifa za Manyara na Tarangire na Burunge inayoundwa na vijiji vya Maweni, Gallapo, Mwinkantsi, Gedamar, Endadosh na Moyomayoka. 

"Wanyama wanaopatikana katika maeneo haya ni simba, swala, twiga, tembo, pundamilia na viboko, hivyo kutokana na baadhi ya wanyama kuwa hatarishi na waharibifu kwa binadamu, mifugo, ndio maana kwa kushirikiana na taasisi hizo, tumewahamisha,” alisema.

No comments

Powered by Blogger.