Full-Width Version (true/false)


Skata la trilioni 1.5 laibuka tena

 
LICHA ya serikali kutoa ufafanuzi kuhusu Sh. trilioni 1.51 ambazo ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2016/17 ulibaini matumizi yake hayaonekani, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema itambana Waziri wa Fedha na Mipango,....... .....Philip Mpango kuhusu suala hilo bungeni jijini Dodoma leo. 

Ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti iliyotolewa Idara ya Habari na Elimu ya Bunge inaonyesha kuwa kwa siku mbili kuanzia leo, kutakuwa na mjadala bungeni kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka ujao wa fedha yatakayowasilishwa na Waziri Dk. Mpango baada ya kipindi cha 'Maswali'. 

Akizungumza na Nipashe jana, Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee, alisema kuwa mbali na mambo mengine, kambi yao imejipanga kuutumia mjadala huo kumbana waziri huyo alieleze Bunge kuhusu matumizi ya Sh. trilioni 1.51 ambazo CAG Prof. Mussa Assad hakuyaona katika ukaguzi wake wa mwaka 2016/17. "Hoja ya matumizi ya Sh. trilioni 1.5 ni lazima tuisimamie maana serikali inasema kuna baadhi ya fedha hizo zimepelekwa Zanzibar," Mdee alisema na kueleza zaidi: "Tunataka kujua uhalali wa matumizi ya hiyo fedha, ilitumika vipi? Bado kuna utata mkubwa sana. 

Hii hoja wachangiaji wa upande wetu wataizungumza. "Ni hoja ambayo bado haijafa na haitakufa kwa sababu PAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali) ambayo ina wajibu wa kusimamia zile hoja zilizoibuliwa katika ripoti ya CAG, itafanya zaidi lakini hatuwezi kuikwepa hoja hii kwenye mjadala wa Wizara ya Fedha." Ijumaa Aprili 20, Bunge lililazimika kusitisha kipindi cha 'Maswali' na kuruhusu serikali itoe kauli bungeni kuhusu hoja hiyo ya matumizi ya Sh. trilioni 1.51 iliyozua gumzo nchini. Akitoa kauli ya serikali bungeni siku hiyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema Sh. bilioni 697.9 zilitumika kulipa hati fungani, Sh. bilioni 689.3 ni mapato tarajiwa na Sh. bilioni 203.9 ni mapato yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Alieleza kuwa katika uandishi wa taarifa ya CAG ya mwaka 2016/17, kulitumika taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa za utekelezaji wa bajeti na kwamba hadi Juni 2017, mapato yaliyokusanywa yalikuwa Sh. trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa Sh. trilioni 23.79. "Matumizi haya hayakujumuisha Sh. bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za serikali zilizoiva," Dk. Kijaji alisema na kufafanua zaidi: "Matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika, hivyo basi baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia ridhaa za matumizi (exchequer issues) yalikuwa Sh. trilioni 24.4." Naibu waziri huyo alisema katika kipindi cha mwaka wa 2012/2013 hadi mwaka 2016/2017, serikali ilikuwa katika kipindi cha mpito cha kutekeleza mpango mkakati wa kuandaa mapato ya serikali kwa kutumia viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma, yaani International Public Sector Accounting Standards (IPSAS Accrual). 

Alisema kuwa katika kipindi hicho, serikali ilitumia mfumo huo kukusanya hesabu za mapato na matumizi ya serikali kuiwezesha kikamilifu kutambua hesabu za mali, madeni na makusanyo ya kodi. Alisema IPSAS Accrual ni mfumo ambao mapato na matumizi yanatambuliwa baada ya muamala husika kukamilika na si hadi pesa taslimu inapopokewa ama kutolewa. 

Alisema matokeo ya utekelezaji wa mfumo huo yameiwezesha serikali kutoa taarifa za uwazi katika taasisi zake na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa mipango. Alisema hakuna fedha ya kiasi cha Sh. trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika bila kuidhinishwa na Bunge, bali ni kutokana na serikali kutumia mfumo huo wa IPSAS Accrual. KUMBANA WAZIRIKatika mazungumzo yake na Nipashe jana, Mdee pia alisema upinzani umejipanga kuutumia mjadala huo wa siku mbili kumbana Waziri Mpango kuhusu utekelezaji duni wa bajeti ya maendeleo katika sekta mbalimbali hasa kilimo, maji, mifugo na uvuvi ambazo zinagusa maisha ya wananchi wengi. 

Mbunge huyo wa Kawe (Chadema) alisema utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa miaka mitatu mfululizo hususan kwenye sekta hizo alizodai zinapaswa kupewa kipaumbele, umekuwa dhaifu. "Tutafanya uchambuzi wa jumla, kwa wachangiaji watakaochangia kutoka kambi yetu, watazungumzia na kutoa tathmini ya utekelezaji wa bajeti za maendeleo katika sekta hizi muhimu zinazogusa wananchi wengi kwa sababu Wizara ya Fedha ndiyo inayopaswa kuzipatia fedha sekta hizi. 

Kwa ujumla, hali ya utekelezaji wa bajeti ya maendeleo si nzuri." TRILIONI 6/- Waziri Kivuli huyo pia alisema hoja yao ya tatu katika mjadala huo ni kutokusanywa kwa fedha za rufani za kodi ambazo zimeshatolewa uamuzi na kutofanyika uamuzi wa kesi za rufani za kodi kutokana na akidi kutotimia. "Kuna changamoto hapa ambayo mimi naona ni uzembe wa mamlaka husika. Kuna zaidi ya Sh. trilioni sita hazijakusanywa," Mdee alisema na kufafanua zaidi: "Kuna Sh. trilioni mbili hazijakusanywa ilhali rufani za kodi tayari zimeshatolewa uamuzi na kuna zaidi ya trilioni nne nazo zimeshindwa kufanyiwa uamuzi ambazo ni kwa faida ya serikali au wafanyabiashara kwa sababu tu ya akidi haitimii kwenye vikao." Alisema hoja yao ya nne ni Wizara ya Fedha na Mipango kutotekeleza Sheria ya Fedha, akieleza kuwa imeshindwa kupeleka fedha kwenye halmashauri. 

Alisema wizara hiyo kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa sasa inakusanya mapato ya halmashauri na inatakiwa kwa mujibu wa sheria kuyarejesha mapato hayo kwenye halmashauri husika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi lakini haifanyi hivyo. 

"Kama unavyojua kila mwaka huwa tunafanya marekebisho kwenye sheria hii ya fedha ili kuendana na mazingira ya mwaka husika. "Sasa, mwaka jana tulifanya marekebisho ya sheria ya fedha na hata mwaka juzi, tukaipa majukumu TRA kukusanya mapato ya taasisi, idara za serikali na halmashauri. "Sheria inaitaka TRA kukusanya kwa niaba ya hizo taasisi na ikipeleka Hazina hizo fedha, Hazina na Wizara ya Fedha kwa ujumla wanatakiwa wazipeleke hizo fedha kwenye halmashauri lakini hawapeleki. 

"Kwa sasa, halmashauri nyingi zina hali mbaya sana kifedha, zina hali mbaya katika utekelezaji wa miradi kwa sababu TRA inakusanya fedha inazipeleka Hazina, lakini Hazina hazirudishwi huku chini. Kwa hiyo, hii ni sehemu mojawapo ambayo tutaiongelea," Mdee alisema.Waziri Kivuli huyo alisema hoja nyingine waliyojipanga kumbana Waziri Mpango kutofanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Deni la Taifa ambayo ina miaka zaidi ya 40 tangu kutungwa kwake. 

Vievile, Mdee alisema kuna changamoto ya kutofautiana kwa takwimu za Deni la Taifa akitolea mfano kuwa hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitaja takwimu za deni hilo zilizotofautiana na za Waziri Mpango ambazo pia hazikuwiana na za CAG Assad. 

"Waziri Mkuu anasema zake, Waziri wa Fedha anasema zake na CAG anakuja na za kwake. Sasa, unavyoona kuna tofauti katika takwimu hizo, ni wazi kwamba kuna shida katika Deni la Taifa," Mdee alisema na kuongeza: "Sheria yenyewe ya Deni la Taifa imepitwa na wakati. Ni sheria ya miaka ya 1970. Hoja yetu hapa ni kwamba miradi tunayoikopea fedha kwa sasa, itarejesha fedha na kulipa deni? "Pia tunaona kuna haja kuruhusu taasisi huru zije kutufanyia 'credit rating' ili itusaidie kama taifa kujua deni letu halisi likoje. 

"Kwa kutofanyiwa credit rating benki nyingi za kimataifa zenye riba nafuu zitaendelea kuogopa kutukopesha kwa sababu hazina uhakika kama tutalipa au la. Matokeo yake tutaendelea kukopa kwa masharti magumu ya kibiashara." Katika ufafanuzi wake kuhusu Deni la Taifa miezi miwili iliyopita, Waziri Mpango alisema kutofautiana kwa takwimu za deni hilo kunatokana na wahusika (Waziri Mkuu, CAG Assad na yeye mwenyewe) kuingiza au kutoingiza deni la sekta binafsi katika ripoti zao.

No comments

Powered by Blogger.