Full-Width Version (true/false)


SMZ yakanusha kuwanyima vibali wawekezaji

 

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekanusha taarifa za kuwapo baadhi ya wawekezaji wanaonyimwa vibali vya ujenzi. 


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Juma Makungu Juma alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swala la mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub. Ayoub alisema licha ya kuwapo kwa kundi kubwa la wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Zanzibar, kuna taarifa kuwa wawekezaji hao wamekosa vibali vya ujenzi. 

Alihoji iwapo Serikali haioni kama kufanya hivyo ni kuwavunja moyo wawekezaji hao? Hata hivyo, Makungu alisema licha ya kuwapo taarifa hizo, katika wizara yake hadi sasa hakuna hata mwekezaji mmoja aliyenyimwa kibali cha ujenzi

Makungu alisema kwa mujibu wa taratibu za utoaji vibali vya ujenzi, maeneo ya uwekezaji ni siku 14 tu. 

“Kama kuna mtu ambaye amechelewa kupewa kibali, basi ifahamike kuwa hajakamilisha utaratibu wetu ikiwamo kuonyesha mchoro wake wa ujenzi wa eneo husika na taratibu nyingine za kitaalamu, ila kwa upande wetu akikamilisha tu ndani ya siku 14 kibali chake kinakuwa tayari,” alisema. 

Alisema kama kuna mwekezaji ambaye amenyimwa kibali cha ujenzi kwa ajili ya uwekezaji, yupo tayari wakati wowote kukutana naye ili kuona ukweli wa jambo hilo. 

Wakati huohuo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed alisema wamedhamiria kufanya utafiti maalumu kujua maeneo yote ya Serikali ili kuyaendeleza na kuyaenzi kwa maslahi ya umma. 

Dk Khalid alisema jitihada zaidi zinaendelea kuyatambua maeneo ya ardhi na majengo ya Serikali ili kuyaboresha na mengine yanaweza kukodishwa kwa watu ambao watakubaliana na masharti yatakayowekwa.

No comments

Powered by Blogger.