Full-Width Version (true/false)


SMZ yataka kuongeza jitihada mapambano dawa za kulevya
Taasisi zinazoshiriki mapambano dhidi ya dawa za kulevya, zimeshauriwa kuongeza ushirikiano ili kufanikisha vita hiyo. 

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mihayo Juma N’hunga alisema hayo juzi alipofungua mkutano wa kutathmini mapambano ya dawa za kulevya kwa miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2018 uliofanyika ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka, Miembeni wilayani Mjini Unguja. 

N’hunga alisema bila ushirikiano wa taasisi zinazohusika na vita hiyo na wananchi, mapambano ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa hivyo kuendelea kuwaathiri vijana wengi na kupoteza nguvu kazi ya Taifa. 

Alizitaka taasisi kuzisoma na kuzielewa sheria kuhusu dawa za kulevya ili kuzisimamia. Naibu waziri huyo alisema bila kuzielewa sheria ni vigumu kufanya kazi kwa ufanisi. N’hunga alisema milango ya Serikali iko wazi kwa wadau wa mapambano ya dawa za kulevya ili kuwapatia ushirikiano wakati wowote. 

Naye mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar, Kheriyangu Mgeni Khamis alisema vita dhidi ya dawa hizo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo maadili kwa baadhi ya watendaji. Alisema kwamba tume itaendelea kutoa elimu kwa wadau ili kila mmoja awe na uelewa. 

Akifunga mkutano huo, naibu katibu mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi alisema vitendo vya dawa za kulevya vinavyoendelea ni aibu kwa Serikali na watendaji waliokabidhiwa dhamana. 

Mitawi alisema Zanzibar imepoteza sifa kimataifa na inaonekana kama uchochoro unaotumika kupitisha dawa za kulevya, jambo ambalo si zuri.

No comments

Powered by Blogger.