Full-Width Version (true/false)


Tanzania imetajwa kuwa nchi iliyofanikiwa


 Tanzania imetajwa kuwa nchi iliyofanikiwa kuwa na mifumo bora ya Teknolojia ya Habari naMawasiliano (TEHAMA) inayolenga kuchochea ustawi wa maisha ya wananchi hasa wanaoishi katika maeneo ya vijijini. 
Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika Jijini Mbeya leo, Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Mawasiliano wa Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) Bw. Desderi Wengaa, amesema kuwa hivi sasa Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano kwa kuwa na mifumo bora na inayoongea, hali inayosaidia kuimarisha huduma kwa wananchi hasa wanyonge. 

"Mifumo hii inalenga kuwawezesha watoa huduma katika ngazi ya vituo vyao kama Zahanati, Shule na Vituo vya Afya kutoa huduma kulingana na mahitaji ya wananchi na vipaumbele vya Serikali ambavyo kimsingi vinalenga kuwaletea wananchi maendeleo endelevu", amesema Wengaa.

Wengaa ameendelea kufafanua kwa kusema "mfumo kama wa Epicor 10.2 utasaidia Serikali kujua mapato na matumizi ya fedha za umma katika sekta za kipaumbele kama Afya na Elimu, ikiwa ni dhamira ya serikali kuhakikisha kuwa rasilimali zote, ikiwemo fedha zinatumika kuboresha maisha ya wananchi".

Aidha, Wengaa ameongeza kuwa kwa kutumia mifumo hiyo, thamani halisi ya fedha zitakazotumika katika miradi ya maendeleo itaonekana na pia itaongeza muda wa kuwahudumia wananchi katika vituo vya kutolea huduma, kwakuwa muda utakaotumika kwa kila anayehitaji huduma kuwa mchache.

PS3 ni mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).  Mradi huo wa miaka mitano unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania bara.

No comments

Powered by Blogger.