Full-Width Version (true/false)


Tukio la Ubakaji St Florence Lazua Hofu kwa Usalama wa Wanafunzi


Dar es Salaam. Tukio la wanafunzi wa kike wa Shule ya Msingi ya St Florence kudaiwa kunajisiwa na mwalimu, limeongeza hofu ya usalama wa watoto shuleni baada ya matukio mengine kutikisa nchi katika miaka ya karibuni.

Tukio hilo limetokea takriban miaka 13 baada ya familia ya mwanamuziki Nguza Viking kukamatwa kwa kosa la kunajisi watoto wa kike maeneo ya Sinza.

Pia imetokea takriban miaka miwili baada ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Mbogamo mkoani Njombe kumpiga mwanafunzi hadi kupoteza fahamu baada ya kumkuta na simu ya mkononi.

Pia limetokea takriban mwaka mmoja baada ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya kumshambulia mwanafunzi wa kidato cha tatu kwa kosa la ukaidi.

Ni mwaka jana tu wakati wanafunzi 32 wa Shule ya Sekondari ya St Lucky Vincent walipofariki ajalini wakati wakienda shule jirani kwa shughuli za masomo.

Pamoja na tukio la wanafunzi wa Lucky Vincent kuwa la ajali, hofu ya usalama wa wanafunzi wanapokuwa shuleni au ziara za kimasomo sasa limeibuka upya baada ya tukio la St Florence.


Baada ya wazazi wa watoto wanaosoma shuleni hapo kupata taarifa, baadhi waliripoti kituo cha polisi na wengine kwenda shuleni kujaribu kuhamisha watoto wao kwenda shule nyingine.

Lakini bado hawana uhakika na huko waendako.

“Mwalimu ni mtu wa kuaminiwa. Mzazi anapompeleka mtoto shule anajua mwanae yupo mikono salama,” alisema mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alipoulizwa maoni yake kuhusu usalama wa wanafunzi shuleni.

“Sasa huyu mtu akianza kuwa mbakaji na mlawiti, hii ni hatari mno, tunapaswa kumsaidia mtoto ajisimamie.”

Alisema njia ya kuwasaidia watoto wa kike ni kuwafundisha ukweli kuhusu ukatili wa kingono, viungo, vyao vya mwili na uwezo wa kusema pale wanapoona dalili za kufanyiwa ukatili huo.

Alisema ni lazima shule za msingi na sekondari ziwe na mikakati ya kuwafundisha watoto namna ya kujinasua kwenye mitego ya wabakaji na walawiti ambao huja kwa sura ya kuwapenda huku wakiwapa zawadi wakati mioyoni mwao wanapanga kufanya ukatili.

“Mtoto akishafikishwa shuleni aambiwe ukweli kabisa kwamba asikubali kuitwa ofisini kwa mwalimu wa kiume kisha mlango wa ofisi hiyo ukafungwa wakiwa wawili tu, wala asikubali zawadi, kukumbatiwa au kuchezewa mwili wake wakiwa faragha,” alisema.

Medesta Kimonga, ambaye ni mtaalamu wa saikolojia wa Chuo cha Ualimu Tanga, anaona matatizo hayo ya ukatili kwa watoto yanatokana na ukosefu wa maadili ya kitaaluma.

“Unakuta mtu huyo alipata kazi kwa sababu hana kazi na hana wito wa ualimu, hivyo haoni mzigo wa malezi isipokuwa kuwajeruhi watoto,” alisema.

Kimonga Alisema athari za watoto kufanyiwa ukatili wa kingono ni nyingi na kubwa ni zile za kisaikolojia.

Kimonga alisema mtoto aliyefanyiwa hivyo na kukosa msaada wa kisaikolojia hukumbwa na ugonjwa wa kuzubaa.

“Ukimpa kazi anaweza kuifanya kwa muda mrefu sana, lakini anaweza pia kupoteza kabisa kumbukumbu,” alisema.

Alishauri jamii nzima kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Naye Venus Kimei, diwani wa Kata ya Mikocheni ambako shule hiyo iko, alisema lazima watoto waambiwe ukweli kwamba wasimwamini mtu yeyote kuwashika miili yao hasa sehemu za siri.

“Wawekewe msingi mzuri wa kukataa wenyewe, lakini baadaye waweze kujieleza kwa wazazi na walezi wanaowaamini,” alisema.

Alisema Serikali inapaswa kuandaa walimu wa saikolojia watakaoweza kuwasaidia watoto shuleni bila kuogopwa.

“Mtoto anapokutana na jambo gumu hasa la kutongozwa na mwalimu, asikae kimya. Ajengewe msingi wa kutoogopa na kutoa taarifa kwa mtu mwingine anayemwamini na atakayemsaidia,” alisema.

Lakini mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Eda Sanga aliwatwisha mzigo wazazi.

“Wazazi wana nafasi kubwa ya kuwajibika kuwasaidia watoto wao kujitambua na kutokuwa waoga,” alisema Sanga.

Alisema katika tafiti mbalimbali walizowahi kufanya waligundua kuwa wengi hufanyiwa ukatili wa kingono na watu wa karibu wakiwamo walimu.

“Wazazi na walezi wasiwe mbali na watoto, wawajengee kujiamini na kupambana na mambo haya wao wenyewe, wapewe uwezo wa kusema wanapokutwa na majanga ya aina hii,” alisema.

Alisema ushirikiano baina ya jamii, walimu, wazazi au walezi na Serikali ndiyo utakaosaidia kutokomeza tatizo hilo.

“Tunahitaji mjadala wa kijamii kujua chimbuko la haya matatizo ni nini? Kuna haja ya kuwatafuta wana saikolojia ili wawasaidie waliofanyiwa ukatili,” alisema.

No comments

Powered by Blogger.