Full-Width Version (true/false)


UFAFANUZI WA KISHERIA:Je ni kweli deni haliwezi kumfunga mtu?

 

 
Ni  kawaida  watu  kukopeshana  fedha  katika  shughuli  za  kibinadamu za kila  siku hasa  zile  za  uzalishaji. Ni  kutokana  na  hili  baadhi  ya  watu  hujikuta  wameingia  katika  faraka ambazo  hata  hivyo  zinatatulika  kisheria. Kwa  wale  ambao  madeni  yao  hutokana  na  taasisi  za  fedha  kama  benki  hawa  huwa  sio  rahisi  kwao  kukwepa kutokana  na  utaratibu  makini  wa  utoaji  wa fedha wa taasisi  hizo. Tatizo  kubwa  la  kutolipana na  kuleteana  dharau huhusisha wadeni  binafsi yaani  mtu  na  mtu. Ni  katika  madeni  haya  ya  watu binafsi  ambamo  msemo  maarufu  wa  deni  halifungi husikika. Ni  kawaida   kukuta  mtu   amekopeshwa  na  hataki  kurejesha  akijiamini  kuwa  deni  halifungi.  Yumkini wapambe  nao  husikika  wakisema,  asikutishe  huyo  deni  halifungi. Kwa  makala  haya  tutapata  kujua  ikiwa  ni  kweli  deni  linafunga  au  halifungi.  

1.KESI  YA  MADAI.

Kesi  za madai  ni  zile kesi   zote  ambazo   si  za  jinai. Kesi  za  madai  hazihusishi  kudaiana  pesa  tu  kama  wengi wanavyojua. Hata  masuala ya  talaka, kudai  fidia, mikataba, madai  ya  vitu  kama  nyumba, magari n.k navyo  huingia  katika  kesi  za  madai. Kwa  hiyo  tunapojiuliza  swali  la  ikiwa  deni  linafunga  au  halifungi  tunaongelea  hivi  vyote. Hata  hivyo  tutajielekeza  zaidi  katika  kudaiana  fedha.

2.     JE  INARUHUSIWA  KUPELEKA  KESI  YA MADAI  POLISI ?.

Unayo  haki  ya  kufungua  shauri ikiwa   kuna mtu unamdai lakini kwa sharti kuwa   shauri  lifunguliwe  pahala stahiki. Wapo  ambao  hupeleka  kesi  za  namna  hii  polisi  japo  huko  si  mahali  pa  kesi  za  namna  hii. Polisi  hujitahidi  kuzitafutia  ufumbuzi   ambapo  wakati  mwingine  hufanikiwa  na  wakati  mwingine  hushindwa. Ukweli  ni  kuwa  kisheria  polisi  hawana  ruhusa  ya  kushughulikia  kesi   za  madai  hasa  hizi  za  kudaiana  hela  na  hata  mali. Ni  basi  tu  wanaamua  kuzishugulikia  lakini  si  kazi  yao kisheria. Madhara  utakayoyapata  utakapomfungulia  kesi  mdai  wako  polisi  ni  pamoja  na  kupoteza  mda  bila  kupata  ulichokitaka.  Hii  ni  kwasababu  mdaiwa  atakapokataa  kutoa  ushirikiano wowote,  polisi  hawana  la  kumfanya. 

Hawawezi  kumfunga  kwasababu  hairuhusiwi. Hawawezi  kumpeleka  mahakamani  kwasababu hawaruhusiwi  kupeleka  kesi  za  madai  mahakamani. Kwahiyo  mdaiwa  uliyempeleka polisi  akiamua  kukomaa  hawana  la  kufanya   utakuwa  umepoteza  muda  na  gharama.

Basi ieleweke  kuwa  kesi  za  madai    kama  haya hutakiwa  kufunguliwa  mahakamani. Yaweza kufunguliwa   mahakama  yoyote  kutegemea  na  kiwango  cha  fedha  unachodai. Waweza  kufungua  mahakama  ya  mwanzo, ya wilaya  na  hata  mahakama  kuu. Usipeleke kesi  ya  namna  hii polisi  labda  kama  unalenga  kumtisha  mdeni  na  si  kupata  haki.

3.  JE   DENI  HALIFUNGI  KISHERIA  ?

Hapana,  deni  linafunga. Ikiwa  utashitakiwa   kwa  kudaiwa  fedha  na  hukumu  ikatolewa  kuwa  unatakiwa  kulipa  hizo  fedha  basi   unatakiwa  uzilipe. Ikiwa  hauna  basi  itaangaliwa  kama  una  mali  kama  nyumba,  gari  au  mali  yoyote ambayo  inaweza  kukamatwa  ili  kulipia  deni. Ikiwa hauna nyumba ,  gari  au  mali  nyingine  yoyote  inayoweza  kufidia  deni  basi  itatakiwa  ukamatwe   ufungwe  kwa  ajili  ya  deni  hilo.  Kifungu  cha  44 ( 1 ) cha  sheria  ya  mwenendo  wa  mashauri  ya  madai kinasema  kuwa  mdaiwa  anaweza  kukamatwa  katika  muda  na  siku  yoyote , na  haraka  kufikishwa  mahakamani ,  na  kuwa  mahakama  inaweza  kutoa  amri  ya  kuwekwa  kizuizini/kufungwa.  Kwa  hiyo  deni  linafunga  labda  mdai  asiamue  kuchukua  hatua.

4.   JE  UKIFUNGWA  DENI  LINAISHA ?.

Hapana  ukifungwa  deni  haliishi. Kifungu  cha  46 ( 2 ) cha  sheria  ya  mwenendo  wa  mashauri  ya  madai  kinasema  kuwa  mdaiwa  aliyeondolewa  katika  kifungo  kwasababu  yoyote  ile,  iwe kwa  kumaliza  muda, ugonjwa  au  vinginevyo  hatahesabika  kuwa  ameondolewa  katika  deni  kutokana  na  kuachiwa  huko.  Hii  ina  maana  unatumikia  kifungo  kikiisha  deni  linabaki  palepale. 

Kifungo hakifuti  au  kusimama    badala  ya  deni  isipokuwa  ni adhabu  ya  ukorofi.  Ni  kutokana na mtazamo  huo wa  sheria  unaolazimisha kutakiwa  kulipa  deni hata  baada  ya  kutumikia  kifungo.  Ukishindwa mara nyingine  tena  kulipa  mdai  anayo  haki  ya  kukurudisha  tena mahakamani  ambapo  unaweza  kufungwa  tena. Msimamo  wa  sheria  ni  mpaka  ulipe  tu.

5.  KULIPIWA  DENI UKIWA  JELA.

Muda  wowote  mdaiwa  akiwa  jela  anatumikia  adhabu  yake  ya  deni  anaweza  kuondolewa  na  kufutiwa  adhabu  hiyo  iwapo  kiwango  cha  deni  analodaiwa  kitalipwa. Mahakama   iliyotoa  amri   ya  kufungwa  ndiyo  itakayotoa  amri  ya kuachiwa baada ya  deni kulipwa katika  ukamilifu wake.

No comments

Powered by Blogger.