Full-Width Version (true/false)


Uongozi St. Florence wamruka mwalimu tuhuma za utomasaji

 


UONGOZI wa Shule ya St. Florence Academy, Dar es Salaam,  umesema haujui aliko Mwalimu Ayubu Mulugo, anayetuhumiwa kudhalilisha wanafunzi, hivyo kuomba  wananchi kutoa ushirikiano ili kumpata na hatimaye  sheria ichukue mkondo wake. 

Uongozi huo umesema umesikitishwa na tukio hilo ambalo ni la kwanza kutokea tangu kuanzishwa kwa shule hiyo miaka 25 iliyopita. Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Shule hiyo, Flora Assey, ilisema uongozi, wazazi na walezi wamesikitishwa na taarifa hizo. 

“Hii ndiyo mara ya kwanza mwalimu wa shule yetu ambayo ilianzishwa zaidi ya miaka 25 iliyopita kupatwa na tuhuma kama hizi na tumekuwa tukijitahidi kuajiri walimu makini na kujenga imani kwa wazazi na jamii nzima kwa ujumla,” alisema Assey. 

Alisema uongozi wa shule hiyo umetoa ushirikiano mkubwa kwa Jeshi la Polisi ambalo linachunguza suala hilo na tayari uongozi na kamati ya shule umekutana na kukubaliana kutekeleza masuala kadhaa.


“Tunapenda kuwatoa hofu kuhusu taarifa zilizozagaa hivi karibuni kuwa shule imemficha mwalimu huyu anayetuhumiwa kwani hata sisi hatujui aliko na tunaendelea kushirikiana na polisi katika suala hili,”alisema. 

 huyo alisema baadhi ya mambo waliyoazimia kufanya ni kuongeza kamera za CCTV katika sehemu mbalimbali za shule ili kuimarisha usalama. Pia alisema wamekusudia kuimarisha uchunguzi wa ndani na kuimarisha kitengo cha ushauri ili wanafunzi wapate usimamizi wa karibu na waendelee kupata ushauri pale inapohitajika. “Uongozi wa shule ya St. Florence tunatoa rai kwa wazazi wote wawe na subira wakati huu ambao polisi wanaendelea na uchunguzi na shule itatoa ripoti mara kwa mara kuhusu suala hili,”alisema Assey. 

Mkurugenzi huyo pia alisema shule inaendelea na maandalizi ya mtihani wa darasa la saba na kuwataka wazazi na walimu washirikiane na uongozi kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana. 

Jumatano ya wiki iliyopita katika mitandao ya kijamii kulisambaa taarifa za mwalimu huyo kudaiwa kuwadhalilisha wanafunzi wa kike wa darasa la saba shuleni hapo kwa kuwatomasa na kuwashika baadhi ya maungo ya mwili. 

Akizungumza na waandishi wa habari siku hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Wilson Kakanga, aliiomba jamii iwe tulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea kuchunguza tuhuma hizo dhidi ya mwalimu huyo ili hatua stahiki zichukuliwe.

No comments

Powered by Blogger.