Full-Width Version (true/false)


Uturuki wana matumaini makubwa na ujenzi wa reli

UBALOZI wa Uturuki nchini Tanzania umesema unaamini kazi ya ujenzi wa Reli ya kisasa unaofanywa na Kampuni ya Yapi Merkez kutoka nchini Uturuki utakamilika ndani ya muda uliopangwa.


Amesisitiza kampuni ya Yapi Markez inao uwezo mkubwa katika masuala ya ujenzi wa reli na hivyo hana shaka kuwa watakamilisha ujenzi wa reli ya kisasa kwa wakati muafaka.Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa  Uturuki nchini Tanzania Ali Govutoglu baada ya futari iliyoandaliwa na Shirika la Ndege la Uturuki kwa ajili ya wateja wake pamoja na mabalozi mbalimbali.


Govutoglu amefafanua uwezo wa kampuni hiyo, si tu unatambulika nchini Uturuki pekee bali dunia nzima katika eneo hilo la ujenzi wa reli.
Hivyo amesema Serikali ya Tanzania haikukosea kwa hatua yake ya kuipa zabuni kampuni hiyo iliyopewa jukumu la ujenzi wa reli hiyo ya kisasa’Standard Gauge’ kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.


"Sina shaka hata kidogo kuhusu kukamilika kwa mradi huu kwa wakati, Yapi Merkez ni kampuni kongwe na yenye ujuzi wa juu katika masuala ya ujenzi wa reli.


" Kwa nchi nyingi ambazo kampuni hii imepewa kazi ya kujenga reli ilitekeleza kwa wakati, hivyo kwa Tanzania ni imani yangu wataliona hilo na kuungana na hiki ninachokisema,"amesema Dovutoglu.


Ujenzi wa reli hiyo utakapokamilika unatarajiwa kuwa suluhisho katika usafirishaji wa abiria na mizigo. Awamu ya pili ya ujenzi umehusisha   kilomita 336 kuanzia Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma huku kampuni hiyo ikipewa tena jukumu la ujenzi huo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema jumla ya wakandarasi 15 walijitokeza baada ya zabuni kutangazwa lakini kampuni hiyo ya Yapi Merkez ndiyo iliyoonekana kukidhi vigezo vya kiufundi na kifedha na majadiliano hayo yalifanyika kati ya Mei hadi Septemba 25 mwaka jana.Amesema ujenzi huo wa treni itakayotumia umeme kuanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro unatarajiwa kuigharimu Serikali Sh. trilioni 2.8.


Wakati awamu ya pili ya ujenzi huo kutoka Morogoro hadi Makutupora ukigharimu Sh.trilioni 4.3 hadi kumalizika kwake.Aidha ujenzi huo kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro utahusisha makaravati matano wakati Morogoro hadi Makutopora yatakuwa 143, huku madaraja kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yakitarajiwa kuwa  24 wakati kuanzia Morogoro hadi Makutopora ni 223.Kukamilika kwa ujenzi huo kutaiwezesha treni kusafiri kwa mwendokasi wa  kilometa 160 kwa saa.

No comments

Powered by Blogger.