Full-Width Version (true/false)


Waandishi Uganda hofu tupu, tozo la kodi ya WhatsApp lawashitua

Shirika la kimataifa la waandishi wa habari wasio na mipaka limelaani kikwazo cha kukusanya taarifa na kuripoti nchini Uganda kufuatia sheria mpya inayotoza kodi ya kila siku kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii. 

Tangu Julai Mosi watumiaji wa mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, WhatsApp, Skype na mitandao mingine watapaswa kulipia kodi ya kila siku ya kiasi cha dola 5 za Marekani ili kuweza kuendelea kutumia huduma hizo. 

Mei 30 mwaka huu Bunge lilipitisha sheria hiyo ambayo Raisi Yoweri Museven amesema ni kwa lengo la kudhibiti habari za kughushi mitandaoni. 

Miongoni mwa walioguswa na sheria hiyo ni wamiliki wa blogu na waandishi wa habari ambao bado wanatumia mitandao ya kijamii kujieleza kwa uhuru zaidi kuliko katika vyombo vingine vya habari nchini humo. 

Mmoja kati ya wamiliki wa blogu maarufu yenye ushawishi nchini Uganda, Rosebell Kagumire ameliambia shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka kuwa katika mazingira ya kunyimwa uhuru wa vyombo vya habari mitandao ya kijamii imetumika kama jukwaa la mijadala ambayo imekuwa ikikosoa Serikali ya Raisi Museven. 

Hayo yanakuja ikiwa imepita miezi michache tangu Mamlaka ya Mawasiliano nchini Uganda (UCC) kusimamisha leseni ya vituo zaidi ya 23 vya redio kwa madai kuwa vimekuwa vikihamasisha uchawi. 

Kwa mujibu wa msemaji wa mamlaka hiyo, Pamela Ankunda vituo hivyo vilifungwa kwa kushiriki katika kuhamasisha na kutangaza vitu vinavyohusiana na uchawi, kufadhili na kukiuka sheria za kimtandao. Vituo hivyo ni pamoja na Metro FM, Nile FM, Kagadi Broadcasting Services, Emambya FM, Village Club FM, Radio Kitara, Packwach FM and Tropical FM. 

Vituo vingine ni Apex FM, Bamboo FM, Ssebo FM, Eastern Voice FM, Eye FM, Victoria FM, RFM, Kiira FM, Tiger FM, Greater African Radio, Dana FM, Gold FM, Hits FM and Radio 5. Kifungu cha 41 (ibara ya 1a na b) ya sheria ya mawasiliano ya Uganda ya mwaka 2013, imeipa mamlaka tume ya mawasiliano kusimamisha au kufuta leseni ya chombo chochote cha habari katika misingi ya kufanya makosa yanayojirudia. 

Ankunda alisema kuwa vituo hivyo vya redio vilipewa taarifa kabla ya kufungwa. na kwamba vilikuwa vikifanya kazi chini ya viwango vya utangazaji vilivyowekwa na mamlaka ya mawasiliano UCC. 

Mamlaka ya mawasiliano imeongeza kuwa vituo hivyo vitafunguliwa pale tu vitakapokiri kuwa havitarudia kurusha vipindi vyenye maudhui yanayokatazwa au kufanya vitendo vingine vyovyote vinavyokiuka sheria za kimtandao. 

Msemaji wa UCC amevitaka vyombo vya habari nchini humo kutoa mafunzo kwa watangazaji wao kuhusu vitu vinavyoruhusiwa na vile ambavyo haviruhusiwi ili kuepuka adhabu kama hii siku zijazo.

No comments

Powered by Blogger.