Full-Width Version (true/false)


Wabunge wapigwa marufuku kubeti

 


SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amewaonya wabunge kujihusisha na michezo ya kubahatisha, akibainisha kuwa yeyote atakayebainika akibeti atafikishwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. 

Kiongozi huyo wa Bunge alitoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma juzi jioni alipokuwa akisisitiza hoja iliyotolewa na Mbunge wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga (CCM) kuhusu michezo ya kubahatisha alipokuwa anachangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka ujao wa fedha. 

Katika hoja yake, mbunge huyo aliitaka serikali kuchukua hatua kudhibiti kasi ya matangazo ya michezo hiyo nchini kwa kuwa ina madhara makubwa kwa jamii, hususan kwa vijana. 

Mlinga alisema michezo ya kubahatisha imepunguza nguvukazi ya taifa kwa kuwa vijana wengi sasa wanatumia muda wao mwingi kujihusisha nayo badala ya kufanya kazi za maendeleo.

Alisema mbali na kupunguza nguvukazi ya taifa, michezo hiyo imekuwa ikichangia umaskini na kuharibu mipango ya familia kutokana na watu kutumia fedha zao kushiriki michezo hiyo kwa matumaini ya kushinda lakini wengi wao hukwama. Kutokana na kauli hiyo, Spika alimuunga mkono mbunge huyo na akisema: "Mbunge yeyote atakayebainika huwa 'ana-bet' atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili". 

MAPATO MENGI 
Katika mjadala huo, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), aliitaka serikali kuongeza kodi kwenye michezo ya kubahatisha kwa kuwa itaiwezesha kukusanya mapato mengi zaidi. Pia alisema bado Deni la Serikali ni himilivu lakini akataka serikali kuendelea kuweka mikakati kuhakikisha deni hilo linaendelea kuwa himilivu. 

Vilevile mbunge huyo aliiomba serikali kuingia ubia na sekta binafsi kwenye miradi mikubwa ya kibiashara ili kuzuia ukopaji wa fedha nyingi kuigharamia. Katika mjadala huo, Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM) alisema kuna haja serikali kutoa fedha za ruzuku kwa halmashauri kwa kuwa kwa sasa miradi mingi iliyo chini ya halmashauri imesimama kutokana na ukosefu wa fedha. 

Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF) aliitaka serikali kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi wa maji yanayotoka Mto Ruvuma kwenda Mtwara Mjini. Maftaha pia aliitaka serikali ieleze kwanini fedha za maendeleo hazitolewi ilhali imeimarisha makusanyo yake. 

Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu (CCM), aliomba serikali kuirudisha iliyokuwa Tume ya Mipango kwa kuwa anaamini bila tume hiyo nchi haiwezi kuwa na uchumi imara. 

Adadi pia aliitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuondoa urasimu katika utoaji fedha za Mradi wa Umeme Vijijini (REA) na Mfuko wa Reli. Mbunge huyo pia aliitaka serikali kutoa fedha za mradi wa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. 

Hoja hiyo ya kutolewa kwa Sh. milioni 50 kila kijiji iliungwa mkono na Suzan Kiwanga, Mbunge wa Mlimba (Chadema), ambaye alihoji tarehe ya kutolewa kwa fedha hizo. Kiwanga pia aliitaka serikali ilipe madeni ya watumishi, wakandarasi na wazabuni wanaotoa huduma ya vyakula kwenye taasisi za umma akibainisha kuwa waliokuwa watumishi wa Tazara Morogoro hawajalipwa pensheni zao licha ya kustaafu miaka ya mapema 2000. 

Katika ufafanuzi wake kwa serikali kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema serikali inaendelea kulipa madeni na kila mtu anayestahiki kulipwa, atalipwa. Alibainisha kuwa katika mwaka huu wa fedha, serikali ilitenga Sh. trilioni moja kulipa madeni lakini mpaka sasa imelipa zaidi ya Sh. trilioni 1.167.

Alisema kuwa kati yake, Sh. bilioni 43 zimelipwa kwa watumishi wa umma 27,589 wakiwamo walimu 15,919. "Tunalipa fedha baada ya kufanya uhakiki kwa sababu bila kufanya hivyo, tutalipa watu wasiostahiki. Mtumishi wa umma anasema anaidai serikali Sh milioni 500 za malimbikizo ya likizo haiwezekani kulipa fedha za aina hii," alisema.

No comments

Powered by Blogger.