Full-Width Version (true/false)


Wanafunzi wa Diploma kuanza kukopeshwa na bodi ya mikopo HESLB


 
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza kuanza kuwakopesha wanafunzi wa stashahada kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq, wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi hiyo uliofanyika mjini Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. 

Alisema Bodi inakamilisha utaratibu huo na utatangazwa mwishoni mwa mwezi Juni, 2018. 

Mkurugenzi huyo alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali kupitia HESLB imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaokopeshwa kutoka wanafunzi 28,383 mwaka 2016/2017 hadi 33,941 mwaka huu wa masomo 2017/2018. Kuhusu urejeshaji wa mikopo iliyoiva, Badru alisema kasi ya kukusanya fedha za mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Mwaka 2015/2016 tulikusanya Sh. bilioni 28 na makusanyo hayo yameongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 13 katika miezi tisa tu ya mwaka wa fedha 2017/2018, yaani Julai 2017 hadi Machi, mwaka huu,” alisema Badru. 

Kuhusu malengo kwa mwaka 2018/2019, Badru alisema serikali imetenga Sh. bilioni 427 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 40,000 na wanaoendelea na masomo zaidi ya 80,000. 

Akifungua baraza hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo, aliwataka watumishi kuzingatia uadilifu na kuimarisha ushirikiano katika utendaji kazi wao. 

“Baraza la Wafanyakazi mahali pa kazi lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kunakuwapo maelewano, ushirikiano na mshikamano kati ya wafanyakazi na uongozi,” alisema Dk. Akwilapo katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. 

Aliongeza kuwa Baraza lihakikishe kunakuwapo na nidhamu ya kazi kwa madhumuni ya kuleta tija na ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za HESLB ili kuhakikisha malengo ya serikali kuanzisha HESLB yanafikiwa kwa ufanisi mkubwa. 

Pamoja na wito huo, Dk. Akwilapo pia aliwapongeza watumishi wa HESLB kwa kutekeleza majukumu yao ya kutoa na kukusanya mikopo ya elimu ya juu kwa ufanisi. 

“Mmekuwa mkifanya kazi kwa bidii na kutoa taarifa kwa umma na hivyo kupunguza malalamiko kwa kuwa wananchi wanaelewa mnachokifanya,” alisema Katibu Mkuu. 

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Dk. Dalmas Nyaoro, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB, Menejimenti na wawakilishi wa Idara na Vitengo vya HESLB. 

 HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 ili kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi Watanzania wasio na uwezo na pia kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na serikali tangu mwaka 1994/1995.

No comments

Powered by Blogger.