Full-Width Version (true/false)


Wazazi wakimbiza watoto shule mwalimu ‘mtomasaji’

 

IDADI ya wazazi wanaowahamisha watoto wao katika Shule ya msingi ya St. Florence Academy, Mikocheni jijini Dar es Salaam imezidi kuongezeka.

Wakati wazazi hao wakifanya hivyo kutokana na taarifa za kuwapo mwalimu Ayubu Mulugo, anayewadhalilisha wanafunzi kwa kuwatomasa na kuwashika sehemu za siri, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, limesema halijawahi kukimbiwa na limeahidi kumtia mbaroni mwalimu huyo. 

Nipashe jana ilishuhudia wazazi waliokuwa nje ya shule hiyo tayari kwa ajili ya kuchukua watoto wao na wengine kuwahamishia shule zingine. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Jumanne Murilo, aliiambia Nipashe jana kuwa Jeshi la Polisi halijawahi kushindwa, hivyo mwalimu huyo atakamatwa hata kama anajifanya amejificha. 

“Tutamkamata, hili ndilo ninaloweza kuwahakikishia wahusika kuwa Jeshi la Polisi halijawahi kukimbiwa. Huyu mwalimu anadhani amejificha lakini nataka kumwambia kuwa mkono wa polisi uko kila mahali. Tutamkamata na wakati wowote tutawapa taarifa za kukamatwa kwake,” alisema.

Jumatano ya wiki hii katika mitandao ya kijamii, kulisambaa taarifa za mwalimu huyo kudaiwa kuwadhalilisha wanafunzi wa kike wa darasa la saba shuleni hapo. Juzi, Jeshi la Polisi lilitanda shuleni hapo ikiwa ni katika kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuwapo. 

Akizungumza na waandishi wa habari siku hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Wilson Kakanga, aliiomba jamii iwe na utulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea kuchunguza tuhuma hizo dhidi ya mwalimu huyo ili hatua zichukuliwe. 

“Yawezekana ni tuhuma au ni kweli lakini hili lina athari kubwa sana kwa watoto na athari huwa za kudumu. 

Kama shule tumepokea habari hizi kwa mshtuko na tayari tumeshalikabidhi Jeshi la Polisi suala hili ili ifanye uchunguzi wake,” alisema. 

Alisema wanaamini Jeshi la Polisi litafanya kazi kwa uwazi na weledi kwa sababu tangu juzi walishinda polisi na jana walifika shuleni hapo. Kakanga alisema kwa upande wake anapigania haki za watoto kwa wanaodaiwa wamefanyiwa vitendo hivyo na wengine ambao hawajui kinachoendelea. 

“Baada ya taarifa rasmi iliyotoka kwa Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Ally Happi, na hii ninayowapa naomba mtuache angalau dakika chache zilizobaki ili tushughulikie mambo ya shule,” aliwaeleza waandishi wa habari. 

Kuhusu madai kuwa uongozi wa shule ulikuwa unafahamu tukio hilo wiki mbili zilizopita, Kakanga alisema jambo linapotokea lazima linyumbuliwe. 

“Tumeshatoa taarifa tunaamini jeshi la polisi kwa weledi wake na uwazi wake watatoa taarifa ya kina kila kinachoendelea na haki itatendeka, tutajua mbichi na mbivu ni zipi,” alisema. 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Hapi, alisema kwa sababu taarifa hizo zimepatikana katika vyanzo mbalimbali hivyo kwa wakati huo wanachunguza ukweli uko wapi.

No comments

Powered by Blogger.