Full-Width Version (true/false)


Waziri Mkuu ampa masaa Waziri Mwijage


 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage aongoze kikao baina ya wabia wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki na menejimenti ya kiwanda hicho na apewe taarifa hiyo leo saa 12 jioni baada ya kufuturu. 

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo jioni Juni mosi, 2018 wakati akizungumza na mamia ya wafanyakazi wa kiwanda hicho mara baada ya kukagua mitambo mbalimbali kwenye kiwanda hicho.

"Serikali haturidhiki na ubia huu, na huyu mbia aelewe kwamba serikali haturidhishwi na ubia huu wala kinachoendelea hapa kiwandani ubia wenu hauna tija. Kwa hiyo wewe Msajili wa Hazina na huyo mwekezaji, nikitoka hapa, mbaki mfanye kikao na mnipe majibu leo saa 12 jioni. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Mkuu wa Mkoa muongoze mjadala huo na nikitoka kufuturu mniambie maazimio yenu, na kama haiwezekani, mvunje kabisa ubia huo ili tujue hatuna mbia tutafute mbia", amesema Waziri Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amesema wabia wakuu wa kiwanda hicho ni Msajili wa Hazina na kampuni ya Changzhou State owned Textile Assets Operations kutoka China na kwamba Serikali ilipoamua kukaribisha uwekezaji ilitarajia kupata mtaji, teknolojia na ajira za kutosha lakini hali ya sasa ni kinyume kabisa.

"Hatuwezi kuvumilia, tunasema tuna mbia mwenye mtaji, hakuna mtaji, tulisema tunataka mbia mwenye kuleta teknolojia mpya, hakuna teknolojia, tulisema aendeshe shughuli hii kukiwa na ajira endelevu, hizo ajira hakuna, halafu tubaki tunamwangalia tu. Bora atuambie amekwama, aondoke, tutangaze vinginevyo.

Tulikopa mtaji lakini Tanzania hizo hela hazijaja, tunataka majibu ya fedha hizo; kama fedha iliyokopwa kwenye Benki ya Exim ya China ingeletwa nchini tungeweza kuziba mapengo na kusaidia kiwanda kiweze kufanya kazi. Sasa kwa sababu fedha hiyo haijaja nchini, tunataka maelezo fedha hiyo iko wapi", amesisitiza Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema kiwanda hicho ni matokeo ya urafiki wa China na Tanzania na kina historia ndefu na mahusiano ya muda mrefu.

No comments

Powered by Blogger.