Full-Width Version (true/false)


Waziri Ummy Mwalimu ameagiza kuwafikisha muhimbili pacha waliozaliwa wakiwa wameungana mkoani Kagera

 


Waziri wa Afya na Ustawi  wa Jamii Ummy Mwalimu amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuwafikisha haraka Hospitali ya Muhimbili watoto pacha waliozaliwa wakiwa wameungana ili wakafanyiwe uchunguzi. 

Ummy ametoa agizo hilo bungeni leo Juni 5 ambapo amekiri kuwepo kwa pacha walioungana waliozaliwa katika kituo cha Misenyi mkoani Kagera. 

Hata hivyo, mama wa pacha hao Jonesia Jovitus yupo Muhimbili tangu Februari mwaka huu. Akizungumza na MCL Digital, mama wa pacha hao, Jonesia amesema kwa sasa yupo MNH na huenda akasafirishwa kwenda Saudi Arabia, mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya watoto hao kutenganishwa. 

Ummy alikuwa anajibu swali la mbunge wa Viti Maalum Suzan Lyimo ambaye ametaka kujua kama serikali inazo taarifa kuwa katika mkoa wa Kagera kuna watoto pacha waliozaliwa wakiwa wameungana. 

“Ni kweli tunazo taarifa hizo na tayari tulishatoa maelekezo kwa mganga wa mkuu wa mkoa wa Kagera ili afanye haraka watoto hao wafike Muhimbili kwa uchunguzi na kuona kama tunaweza kuwatenganisha, lakini niwaambie Watanzania kuwa mahali popote wanapozaliwa watoto wa aina hiyo watoe taarifa na hatua zichukuliwe mapema,” amesema Mwalimu. 

Pacha kama hao, Maria na Consolata wamefariki juzi, baada ya kuugua kwa muda mrefu na wanatarajiwa kuzikwa kesho, Iringa.

No comments

Powered by Blogger.