Full-Width Version (true/false)


Yanga kubeba nyota wanne Gor Mahia

 


Mabingwa wa kihistoria wa soka Tanzania Bara, Yanga wanatajwa kuwa katika harakati kuibomoa klabu ya Gor Mahia, inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Mwingereza Dylan Kerr. 

Kwa mujibu wa mtandao rasmi wa klabu ya Gor Mahia ni kwamba, baada ya kutupwa nje kwenye michuano ya SportPesa Super Cup, Yanga wamepania kusuka upya kikosi chao na katika harakati hizo wamewalenga nyota wanne wa Gor Mahia. 

Taàrifa hizo zinadokeza kuwa uongozi wa Yanga, ikiongozwa na Kocha wake, Mkongomani Zahera Mwinyi, inataka kuwasajili wachezaji wanne wa Kogalo ambao ni beki Godfrey Walusimbi, kiungo mchezeshaji Francis Kahata, straika Meddie Kagere na kiungo mshambuliaji George Odhiambo 'blackbery'.

Hata hivyo, Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr alipuuzia mbali taarifa hizo na kusisitiza hakuna mchezaji yeyote atakayenyanyua mguu kuondoka klabuni hapo kwa sasa kwa gharama yoyote huki akidokeza kama kuna dili la usajili basi itakuwa ni kuongeza mchezaji na sio kuruhusu mchezaji aondoke. 

"Eti nini? Hilo halipo, haliwezi kutokea na haitotokea. Kwa sasa tuna ratiba ndefu na ngumu, tuna mechi takribani 65 za kushughulikia, kama kuna dili lolote la usajili basi itakuwa ni kuongeza mchezaji na sio kuuza," alisema Kerr. 

Gor Mahia na Yanga watakutana katika mchezo wa tatu wa makundi, Kombe la Shirikisho Afrika, utakaopigwa Julai 17, mwaka huu, katika Uwanja wa Kenyatta, mjini Machakos nchini Kenya. Mbali na nyota hao, taarifa zinasema kuwa, tayari Yanga wameshaonesha nia ya kumtaka kiungo wa AFC Leopards, Whyvonne Isuza. Kama sajili hizi zitatokea basi amini usiamini kikosi cha Yanga kitatisha sana. 

Ikumbukwe kuwa hii sio mara ya kwanza kwa klabu ya Tanzania kuchukua mchezaji kutoka Kenya kwani mabingwa wa sasa ligi kuu ya Vodacom, klabu ya Simba iliwahi kumchukua mchezaji kutoka Gor Mahia kwa jina la Dan Sserunkuma na Donald Mosoti, Azam ilikuwa na Allan Wanga bila kusahau miaka ya nyuma, Boniface Ambani aliamsha dude pale Jangwani.

No comments

Powered by Blogger.