Full-Width Version (true/false)


Yanga yafanya umafia Michuano ya CAF

 

YANGA buana wana michezo ya hatari sana. Achana na matokeo yake ya jana ya kupigwa mabao 3-1 na Kakamega Homeboys pale uwanjani Afraha mjini Nakuru. 

Mabosi na benchi la ufundi la Yanga linawaza mbali kwelikweli na wala hawakuwa na mpango wa kwenda England kukipiga na Gor Mahia wala kusaka Dola 30,000 (Sh68 milioni) kwenye SportPesa Super Cup. 

Iko hivi sasa. 
Si unafahamu mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu wanashiriki mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na wamepangwa na Gor Mahia, ambayo pia iko mjini Nakuru. Sasa akili na harakati za Yanga ni kutekeleza miakakati ya kusaka ushindi ikiwa ni pamoja na kupepeleza taarifa muhimu za wapinzani wao, Gor Mahia wanaoshika nafasi ya pili kwenye kundi lao.  

Yanga ambayo ipo mkiani mwa kundi hilo ikiwa na pointi moja, itacheza na Gor Mahia baadaye mwezi ujao hivyo benchi la ufundi la timu hiyo limejiweka sawa likipiga hesabu kali ili kunasa taarifa za kishushushu za wababe hao wa soka la Kenya. 

Kocha Msaidizi wa Yanga, ambaye ndiye anakaimu nafasi ya Kocha Mkuu kwa sasa, Noel Mwandila alisema wanafahamu kuwa Gor Mahia imeficha kikosi chake kamili kwenye michuano hii, lakini wana uhakika wa kunasa ishu zao zote muhimu. 

Amesema nyota wote wa Gor Mahia ambao hawajajumuishwa kwenye michuano hiyo ya SportPesa, lakini watanasa kila kitu kabla ya kurejea nchini. Mwandila alisema tayari walishaanza kukusanya taarifa za Gor Mahia kwa kutazama mechi zake mbili zilizopita za hatua ya makundi, lakini pia michuano hii ya SportPesa itawasaidia zaidi. “Tunafahamu Gor Mahia ni wapinzani wetu wakubwa kwenye hatua ya makundi. 

Bado hatujakutana nao hivyo hii ni fursa muhimu kwetu kupata taarifa zao,” alisema Mwandila. “Hatukuja kwenye mashindano haya ya SportPesa kwa nguvu kubwa, tunalifahamu hilo. Ni ngumu kusema wanavyocheza hapa ndivyo watakavyocheza hapo baadaye kwenye michuano ya CAF. 

“Hata hivyo, hiyo haiwezi kutuzuia kuchukua taarifa zao muhimu. Tunaweza kutazama uwezo wa baadhi ya wachezaji wanaocheza hapa na baadaye tukapata taarifa za timu yote,” alifafanua Mwandila, ambaye anakaimu nafasi hiyo wakati huu ambapo, kocha mkuu Mwinyi Zahera hajatua nchini hapa. 

WAPIGWA 3-1 KIULAINI 
Yanga imeanza kwa unyonge michuano ya SportPesa nchini Kenya baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Kakamega Homeboys, mechi iliyochezwa jana Jumapili, Uwanja wa Afraha, Nakuru. 

Yanga iliyocheza bila mastaa wake, huku straika wa zamani wa Azam FC ambaye sasa anakipiga Kakamega Homeboys, Allan Wanga akipachika mabao mawili dakika ya 26 kwa shuti na ya 30 kwa penalti kabla ya bao la tatu lililowatoa mchezoni. 

 Yanga ilipambana na dakika ya 35 Matteo Anthony aliifungia bao la kufutia machozi kutokana na mpira wa adhabu.

No comments

Powered by Blogger.