ACT-Wazalendo Waitaka Serikali Isitumie Mabavu Kudhibiti Tafiti Zinazofanywa Nchini
Chama
cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kutotumia mabavu kudhibiti tafiti
zinazofanyika nchini badala yake itoke hadharani na kujibu hoja
zinazoibuliwa.
Chama
hicho kimetoa tamko hilo leo Julai 11 baada ya kuiona barua mitandaoni
iliyoandikwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ikiitaka Taasisi
ya Utafiti ya Twaweza kujieleza kwa nini wasiadhibiwe kwa kufanya
utafiti bila kupata kibali chao.
Akizungumza
na vyombo vya habari leo Julai 11 jijini Dar es Salaam, Katibu wa
Itikadi, Uenezi na Mawasiliano, Ado Shaibu amesema ni aibu kwa serikali
kudhibiti mpaka shughuli za utafiti.
"Kama
barua hiyo ni ya kweli, basi ni aibu kubwa kwa Serikali kudhibiti
utafiti. Tutasimama imara kulinda na kutetea hadhi ya utafiti ili mradi
utafiti huo uwe unakidhi vigezo," amesema Shaibu.
Amesema
Serikali isiogope mapambano ya hoja kwa sababu ina watu wengi wanaoweza
kuzungumza na kutetea hoja badala ya kutumia mabavu na kutaka kuiadhibu
Twaweza kwa kufanya utafiti wa Sauti za Wananchi.
Amefafanua
kwamba kwa miaka mingi Twaweza wamekuwa wakifanya tafiti na Costech
walikuwepo, lakini kwa sababu utafiti wao wa hivi karibuni umeigusa
Serikali, wamejitokeza wakisema hawajafuata taratibu.
"Ninavyofahamu
mimi, taasisi yoyote ikitaka kufanya utafiti lazima iwasiliane kwanza
na NBS (Ofisi ya Taifa ya Takwimu). Ni jambo la kushangaza kama utafiti
hauwezi kufanyika kama haujapata approval ya Costech, suala hili
linaibua mjadala," amesema katibu huyo.
Kuhusu
uchaguzi mdogo wa Agosti mwaka huu, Shaibu amesema kamati kuu ya ACT
Wazalendo imeamua kushiriki kwenye uchaguzi huo kwenye nafasi
mbalimbali.
Hata
hivyo, amesema wameunda kamati maalumu ya mashauriano itakayoongozwa na
Omary Shaibu Shaaban ili kushauriana na vyama vingine juu ya
kusimamisha mgombea mmoja kwenye maeneo ya kimkakati.
No comments