Full-Width Version (true/false)


Aslay: Hili la Tessy bado linaumiza sana

  

           
KAMA kuna msanii ambaye kwa sasa ameishika Bongo, basi huyu Aslay unaweza kusema anatumia kizizi aisee. Kila kona kwa sasa ni Aslay tu na ilinichukua saa kadhaa kumsubiri ili nipate nafasi ya kupiga stori mbili tatu naye.
Hata hivyo, kama kawaida huwa hatushindwi kitu na Mara Paap Aslay huyu hapa bana.
Si unajua Aslay yupo kwenye anga za juu kabisa kwa sasa na Mwanaspoti likataka kufahamu ishu mbalimbali kuhusu muziki, maisha yake na mapenzi kwani, huko kwenye mitandao kuna balaa kwelikweli mara Tessy, mara Diana basi fujo tupu.
Mtakumbuka milango ya mafanikio ya Aslay ilianza kufunguka baada ya kujiunga na kuanzishwa kwa Yamoto Band akiwa sambamba na Maromboso, Enock Bella na Beka Flavour.
Hapo Afrika Mashariki nzima watu ni Yamoto Yamoto hadi raha unaambiwa.
Lakini, baadaye bendi hiyo ikavunjika na kila mmoja kubeba virago vyake na hapo Aslay akashika kasi zaidi huku akiwatimulia vumbi wenzake.
Kwa sasa kuna ngoma kali zinatamba kama Angekuona, Baby, Mhudumu, Pusha, Likizo, Natamba, Tete, Kwa raha, Hauna, Nyakunyaku, Nibebe na sasa kuna Totoa.
Eti! Kuna ishu za ushirikiana?
Mengi yanasemwa huko kwenye mitandao kuhusiana na kutamba kwa Aslay, lakini mwenyewe amefungukia Mwanaspoti akisema:
“Sina timu au kikundi cha watu kwa ajili ya kufanya fitna ili nionekane bora kwa mashabiki.
Nategemea kazi nzuri kwa timu yangu ya menejimenti ambayo kila kukicha inaumiza kichwa.
“Hadi kufikia hapa tangu nianze muziki huwa sina utamaduni wa kutumia ushirikina wala hongo.
“Uongozi wangu na nguvu ya umma (mashabiki) ndio wamenifanya kuwa Aslay huyu unayeniona. Kila nikitoa ngoma mashabiki wanaikubali na kusapoti kazi.”
Aah! Bado niko naye sana tu
Kuna mengi yanasemwa juu ya Aslay kutemana na meneja wake, ambaye amemtengeneza na kuwa juu kwenye muziki.
Hata hivyo, mwenyewe anakanusha madai hayo akisema kuwa mpaka sasa bado yuko na Meneja Chambuso na hana mpango wa kubadili uongozi kwani, kazi inayopigwa hapo sio ya kitoto kabisa.
“Bado nipo chini ya Chambuso na kamwe sijaondoka kama watu wanavyodai, pia kuna Mc Carter ambaye ni meneja wa biashara wa Shetta,” alisema Aslay.
Kama asingekuwa msanii je?
Kuna watu wamejaliwa vipaji jamani achene tu, kama ilivyo kwa Ali Kiba ambaye uwanjani ni mahiri kama Cristiano Ronaldo na huyu Aslay naye ndo hivyo.
Anasema kuwa kama asingekuwa msanii basi angekuwa anafanya yake pale Uwanja wa Taifa akiwa na Yanga ama Simba kwani ana kipaji cha uhakika katika soka.
Vipi kuhusu Tessy na Diana?
Aslay ambaye pia anafahamika kama Baba Moza, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu na mwanamitindo na video Queen, Tessy ‘Mama Moza’, lakini ghafla tu mambo yakabadilika.
Wawili hawa wamefanikiwa kupata mtoto mmoja, Moza lakini kwa sasa hali imechafuka huku Aslay akidaiwa kuhamishia majeshi kwa msanii wa filamu Diana Kimario na mambo ni moto.
Pia, Tessy naye anadaiwa kuangukia kwenye mikono ya bonge la bwana mmoja hapa jijini, lakini hapa Aslay anafunguka kuhusiana na ishu nzima.
“Huwa sipendi kulizungumzia hili suala kwa sababu linaniumiza sana, ila ukweli ndio huo kama ulivyosikia nimeachana na mama Moza.
“Ni mambo ya familia na kilichobaki kwa sasa ni uhusiano wa wazazi wenye mtoto, ambaye anahitaji uangalizi wa pande zote.
“Unajua kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa hii ni kiki, lakini mimi sio mtu wa kiki kabisa na ninazungumza hapa ni ukweli mtupu,” alisema Aslay ambaye jina lake kamili ni Aslay Isihaka Nassoro.

No comments

Powered by Blogger.