"BASATA haiwezi kunilipa" - Steve Nyerere

Steve amebainisha hayo wakati akizungumza na www.eatv.tv leo
Julai 13, 2018 baada ya wadau mbalimbali wa filamu na muziki
kumshambulia kupitia ukurasa wake wa kijamii kuwa amepatiwa fedha 'fungu
lake' ndio maana anajifanya kutaka kukaa kikao na wasanii wenzake ili
wapate ufumbuzi juu ya jambo hilo ambalo limekuwa gumzo kwa sasa.
"BASATA haiwezi kunipa fedha 'fungu' lolote kwa ajili
yangu mimi huko ni kuichafua, mimi ni nina nguvu gani mpaka wanilipe.
Lazima niwe upande wa wenzangu ambao ni wasanii na msema ukweli siku
zote ni mpenzi wa Mungu, kiukweli milioni tano kwa msanii ni pesa nyingi
sana hata ingekuwa milioni moja bado shida ingekuwepo", amesema Steve
Pamoja na hayo, Steve ameendelea kwa kusema "kama kweli
BASATA walitaka kutusaidia walipaswa waanze kutupa kazi wao kwa
kututengenezea mifereji ya kupata matangazo ili ndio watake hizo pesa
walizozitaka. Kwa namna moja ama nyingine hayo makampuni yakikataa
kutupa matangazo sisi na yakaenda kuwapa raia wa kawaida hao BASATA
watakuwa wanapata nini zaidi ya hasara tu. Duniani kote msanii anapata
fedha kupitia matangazo".
Mbali na hilo, Steve Nyerere ameitaka jamii kutoliingiza suala hilo
katika mlango wa kisiasa licha ya kuwa yeye yupo ndani ya chama cha
Mapinduzi (CCM).
Siku za hivi karibuni Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) liliweza
kufanya mabadiliko mbalimbali katika tozo zao za utoaji wa huduma
ikiwemo ya makampuni kulipa milioni tano kwa BASATA endapo watamtumia
msanii kufanya tangazo la aina yoyote, jambo ambalo limekuwa likipingwa
na wasanii wengi nchini wakidai kuwa kwa kitendo hicho watakosa kazi.
Kupitia kipindi cha Planet Bongo kilichorushwa Julai 10, 2018 na
East Africa Radio, BASATA ilitoa ufafanuzi juu ya suala hilo kuwa sio
kweli kwamba msanii anatakiwa kulipa milioni 5 akifanya tangazo bali
kampuni husika ndio inapaswa kufanya hivyo kwa kuwa wanaingiza kipato
kikubwa kutumia tangazo hilo.
No comments