Full-Width Version (true/false)


Binti wa miaka 15 alia polisi kusambaratisha ndoa yake
Aghalabu watoto wa kike walio wengi wenye umri wa chini ya miaka 18 na waliofaulu kuendelea na masomo ya sekondari, huchukizwa na kitendo cha kuozwa.
Lakini kwa Maria Fimbo, (siyo jina lake halisi) alifurahia kitendo hicho na kulaani polisi waliozuia ndoa yake.
“Nasikitika sana polisi kuingilia sherehe yangu, wameniharibia siku yangu ya harusi na sijui kama mume wangu atarudi tena kunioa,” anasema.
Maria (15), alifunga ndoa ya kimila, Julai Mosi na baadaye sherehe fupi ilifanyika katika ukumbi wa Kijiji cha Bukungu. Hata hivyo, polisi walivamia na kuisambaratisha.
Akizungumza na Mwananchi, Maria alisema baada ya kumaliza darasa la saba Oktoba, 2017 alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Msalala wilayani Nyang’wale mkoani Geita.
“Matokeo yalipotoka niliambiwa nimefaulu na nilienda kuchukua fomu ya kujiunga na kidato cha kwanza, lakini babu aliniambia sitasoma kwa sababu hawana pesa ya kunisomesha hata ya kuninunulia sare za shule, hivyo sijawahi kuingia darasani kabisa,” alisema.
Maria alisema aliamua kuolewa kutokana na familia kuwa na kipato kidogo na mama yake kuwa na mzigo mkubwa wa malezi ya watoto huku akiwa hana uwezo wa kuwasomesha.
Alisema haikuchukua muda kabla ya mwanamume wa kumuoa kujitokeza na babu yake alichukua mahari ya ng’ombe watano na Sh 100,000.
“Nilikubali na nikafunga ndoa lakini sijui hatima yake kwa sababu mume wangu amenikimbia,” alisema msichana huyo ambaye kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 anatambulika kama mtoto. Sheria hiyo inautambua umri wa chini ya miaka 18 kuwa wa mtoto.
Uvamizi wa polisi ukumbini
Maria anasema: “Baada ya polisi kufika ukumbini watu walikimbia, mama yangu, babu na hata mume wangu waliniacha ukumbini ndio polisi wakanichukua.”
Anasema aliwekwa mahabusu kwa siku saba bila kuwaona ndugu zake wakija kumuangalia na baada ya kipindi hicho aliwekewa dhamana.
Binti huyo anasema ofisa tarafa wa Karumwa, Vitalis Ndunguru ndiye aliyemuwekea dhamana na akaachiwa kwa masharti ya kuripoti kituoni hapo kila baada ya siku tatu.
Anasema wazazi wake yaani mama, babu na mume aliyemuoa wametoroka na hawajulikani walipo mpaka sasa.
Familia ya Maria yenye watoto kumi kwa sasa wanalelewa na dada yake Maria, Katherin (siyo jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 20 ambaye hata yeye alifaulu kuendelea na masomo, lakini hakuendelea na kuamua kuolewa.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Msalala, David Maega anasema mwanafunzi huyo alichaguliwa kujiunga, lakini hakuripoti.
Anasema wanafunzi 468 walichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu katika shule hiyo, lakini wasichana 20 na wavulana 19 hawajaripoti mpaka sasa.
Kaimu ofisa elimu wa Shule za Sekondari mkoani Geita, Christopher Makoye anasema kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu za elimu mwanafunzi anaposhindwa kuhudhuria masomo kwa siku 90 bodi ya shule inamuondoa kwa kukosa sifa.
Anasema kwa kuwa babu yake Maria ni mwenyekiti wa bodi ya shule, anaifahamu sheria hiyo na ndio maana akajua mjukuu wake asipohudhuria masomo kwa siku hizo atakuwa amejifukuzisha shule.
“Ndiyo maana walisubiri siku 90 zipite wamuozeshe wakijua mtoto atakuwa hana sifa ya kuendelea na masomo,” anasema mwalimu Makoye.
Anasema babu wa binti huyo (hamtaji jina), anaifahamu vyema Sheria ya Elimu Na.25 ya mwaka 1978 inayozungumzia masuala ya elimu ambapo imeweka wazi kuwa mwanafunzi atafukuzwa shule iwapo hatahudhuria kwa siku 90.
Makoye anasema kwa kipindi cha Januari 2017 hadi Mei 2018, wanafunzi 60 wa sekondari wameacha masomo baada ya kupata ujauzito.
Kadhalika, anasema wanafunzi 309 waliopaswa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu hawajaripoti shuleni, kati ya hao wavulana ni 209 na wasichana ni 100.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Hamimu Gwiyama anasema waliamua kuzuia ndoa hiyo kwa sababu binti huyo alichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, hivyo kimsingi bado ni mwanafunzi.
“Hata kama alikubali kuolewa lakini tunajua sisi, tumechunguza na kujua alidanganywa na wazazi ili wapate mali,” anasema.
Anasema Serikali inatoa fedha nyingi kugharamia elimu, lakini wapo baadhi ya wazazi kwa tamaa ya mali wanawaozesha watoto wao. “Vita hii tutapigana bila kuchoka, yeyote atakayejiingiza kukatisha ndoto za mwanafunzi tutahakikisha tunamchukulia hatua za kisheria na hata hawa waliokimbia waendelee kukimbia, lakini mwisho tutawakamata,” anasema Gwiyama.
Anasema kwa sasa mwanafunzi huyo atapimwa na ikibainika hana ujauzito, atalazimishwa kurudi shuleni.
Mkuu huyo wa wilaya anawataka watoto kutojiingiza kwenye mapenzi wakiwa wadogo kwani licha ya kuharibu ndoto zao za baadaye, pia wanakuwa kwenye hatari ya kupata saratani ya mlango wa kizazi.
Mkanganyiko wa kisheria
Akizungumzia tukio hilo, Wakili Onesmo Kyauke anasema tatizo linaanzia katika dini, ambapo baadhi ya dini zinaruhusu watoto wa kike kuolewa pindi wanapovunja ungo.
Hata hivyo, anasema jamii imeanza kubadilika na sasa watoto wa kike wana fursa zaidi ya kusoma tofauti na zamani walipokuwa wakinyimwa na jamii zao.
“Lakini katika suala hili la Maria, nadhani kuna ukinzani wa kisheria. Kama binti ana nafasi ya kusoma, hapo sheria ya mtoto inamlinda kwa sababu amenyimwa elimu. Lakini kwa yule ambaye hakuendelea na shule, sheria ya ndoa inamruhusu (kuolewa),” anasema wakili huyo. Kyauke anasema waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi aliizungumzia kwa kina sheria hii akiwa bungeni na kusema inahitaji majadiliano ya kina kabla ya kurekebishwa.
Wakili huyo anasema sheria hiyo inagusa ndoa ambazo hufungwa kulingana na dini tofauti pamoja na watu ambao hawana dini.

No comments

Powered by Blogger.