Full-Width Version (true/false)


DC akana mauaji kuhusishwa Al-Shabab
MKUU wa Wilaya ya Tanga,Thobias Mwilapwa, amesema matukio ya kuuawa kinyama watu watatu akiwamo mwanamke aliyebakwa kabla ya kuchinjwa wiki iliyopita ni ya kawaida na hayahusiani na kikundi cha Al-Shabab. 


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mwilapwa alieleza kuwa matukio hayo yanafanywa na wahalifu wa kawaida na kuwatoa wananchi hofu kuwa yanafanywa na kikundi maalumu cha mauaji (Al-Shabab). 

Mwilapwa alikuwa akitoa taarifa ya serikali kuhusiana na hali ya usalama Wilaya ya Tanga kutokana na matukio hayo na kueleza kuwa mauaji hayo hayana uhusiano wowote na yaliyotokea Kibatini ya watu wanane kuchinjwa kama kuku Machi, 2016 na kutikisa taifa. 

Mwezi huu watu watatu akiwamo mwanamke mfanyabiashara, Hidaya Shaban (34) aliyekuwa mkazi wa mtaa wa Japan jijini hapa, anasadikiwa kufanyiwa vitendo vya ubakaji kabla ya kuchinjwa hadi kufa na kuzusha hofu kubwa kwa wananchi jijini hapa. 

 “Kuna watu wameanza kuhusisha mauaji haya na yale ya Kibatini ya watu wanane kuchinjwa usiku…matukio haya hayana uhusiano… huu ni uhalifu wa kawaida tu,” alisema Mwilapwa. 

Alieleza kuwa vifo hivyo kwa nyakati tofauti vimehusisha watu watatu na siyo saba kama inavyovumishwa na kutaja mitaa iliyohusika na mauaji hayo kuwa ni Magaoni, Masiwani Shamba na Kivumbi Tifu. 

“Watu watatu wameuawa katika matukio saba tofauti yaliyotokea katika mitaa hiyo…na taarifa ya serikali ni kwamba huu ni uhalifu wa kawaida auhusiani na tukio la Kibatini,” alisisitiza Mwilapwa. 

Hata hivyo, katika kikao hicho, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kama kawaida na kueleza kuwa tayari serikali imeshadhibiti wahalifu hao ikiwamo kuwakamata watu zaidi ya 10 wanaohusishwa na matukio hayo. 

Akielezea hatua za serikali kukabiliana na uhalifu huo, alisema kuwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi wa maeneo hayo pamoja na wananchi kwa ujumla na kuimarisha ulinzi shirikishi kwenye mitaa yote ya Jiji la Tanga.

No comments

Powered by Blogger.