Full-Width Version (true/false)


Fei Toto atabiriwa makubwa
MASTAA wa Yanga wamemfanyia wepesi kiungo mpya wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoona ugumu wa maisha atakayoyaanza klabuni hapo kwa kumwambia atafika mbali kisoka.
Mastaa hao wa Jangwani wamefunguka kuwa, Toto ana vitu vingi vya dhahabu kwenye miguu yake na kwamba, amechagua mahali sahihi panapoweza kumfanya akafika mbali.
Beki wa timu hiyo, Haji Mwinyi, alisema ni kawaida kwa mchezaji kuanza moja anapotua timu mpya hasa pale unapokutana na wachezaji wapya, lakini kwa Fei Toto hilo ni rahisi kwani atapewa ushirikiano wa kutosha.
“Dogo ni fundi naamini ushirikiano wetu utaonyesha zaidi madini aliyonayo, kikubwa atulize akili na abadilishe mtazamo kujua Yanga ni klabu yenye mashabiki wenye kiu ya mafanikio zaidi,” alisema
Emmanuel Martin ni winga wa timu hiyo, alikiri kuwa Fei Toto ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa hivyo ujio wake Yanga umeongeza nguvu nyingine na kuahidi kumpa ushirikiano wa kuonyesha ufundi wake.
“Ushirikiano tutakaompa ndio utakaomjengea ujasiri wa yeye kucheza kwa kujiamini na kwa faida ya klabu, bila shaka mabosi wanasajili kwa malengo ya mafanikio ya kutwaa ubingwa msimu ujao,” alisema.
Aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Sekilojo Chambua, alisema umri wa mchezaji huyo na uwezo anaouonyesha utakuwa na manufaa kwa Yanga, huku akisisitiza ushirikiano na umoja ndio silaha kubwa.
“Ana vitu adimu mguuni kwake ambavyo vikijengewa uzoefu vitakuwa faida kwa Yanga, wachezaji aliowakuta ndani ya timu wampe ushirikiano wa kutosha wakizingatia wapo kwa ajili ya klabu na sio maslahi binafsi,” alisema.

No comments

Powered by Blogger.