Full-Width Version (true/false)


Hakuna mtu anayejiua mwenyewe, jamii ndio humuua kwa namna hii
Polisi watatu wamejiua ndani ya saa 48 katika matukio ambayo yameripotiwa nchini, hivyo kuleta mshtuko miongoni mwa wananchi wa kawaida.
Ni mfululizo wa matukio ya watu ama kujiua au kuua watu wengine kwa sababu mbalimbali ambayo yametawala nchini ndani ya miezi michache.
Siku mbili zilizopita tumeshuhudia matukio ya polisi watatu kujiua huku wakipishana kwa saa chache, huku miezi ya karibuni matukio ya watu kujiua au kuua wengine yakiripotiwa zaidi kwenye vyombo vya habari.
Jambo la muhimu ambalo tunapaswa kukumbuka ni kuwa polisi ni binadamu kama walivyo raia wengine wa kawaida.
Kwa sababu hiyo basi, kama jambo linaweza kufanywa na raia wa kawaida, isiwe jambo la kushangaza jambo hilo likifanywa na polisi.
Hata hivyo, inaweza kuibuka hoja kuwa polisi wanafundishwa ujasiri hivyo hawatakiwi kujiua au kujinyonga. Ubinadamu wao unabaki palepale.
Zimekuwa zikitolewa sababu nyingi za watu kujiua au kujinyonga, wataalamu wa saikolojia na sosholojia wamekuwa wakizitaja sababu hizo ingawa nao wakati mwingine wamekuwa wakikinzana.
Sababu zinazotolewa mara kwa mara kama chanzo cha watu kujiua ni wivu wa mapenzi, ugomvi, ulevi, mateso, ugonjwa, kufilisika, ugumu wa maisha na mambo mengine kama hayo.
Ukifuatilia kwa kina, utakubaliana kuwa sababu nyingi ambazo hutolewa huwa ni vichocheo zaidi, ingawa huwa kuna sababu za msingi na ndio chanzo hasa.
Sababu kubwa na ya msingi ambayo huwafanya watu kujiua ni kudhani jamii na dunia imewakataa. Mtu anapofika hatua akaamini kuwa hakubaliki kwa kila mtu, huona dunia imemkataa na hivyo njia rahisi kwake huwa ni kutafuta msaada mwingine ambao huwa ni kujiua kwa njia yoyote ama kujinyonga, kujipiga risasi au kunywa sumu.
Emile Durkheim, Mfaransa aliyeishi kati ya mwaka 1858-1917 na kuweka misingi ya sayansi ya jamii alifanya utafiti kutaka kujua chanzo cha watu kujiua baada ya kuona tatizo kubwa barani Ulaya.
Mtaalamu huyo wa sosholojia, anasema sababu kubwa ya mtu kujiua huwa ni ya kijamii na si mtu binafsi. Kwa maana nyingine ni kuwa mfumo katika jamii husababisha mtu mmoja mmoja kujiua.
Durkheim, ambaye mwaka 1897 alichapisha kitabu kuonyesha msisitizo kuwa sababu za kujiua si za mtu binafsi ila ni za kijamii, ameweka makundi manne ya vifo vitokanavyo na watu kujiua wenyewe.
(i) Anomic suicide: Anasema kundi hili huhusisha watu wanaodhani wametengwa na jamii yao huku mifumo katika jamii ikiwa legelege. Anasema watu wanapoona hakuna sheria, hakuna utamaduni, mila wala desturi huwa wanachanganyikiwa. Matatizo ya kijamii, kiuchumi, mapinduzi ya kisiasa ambayo kwa ujumla hubadilisha mfumo wa maisha ya kila siku huwa inawachanganya baadhi ya watu na kutokana na mabadiliko hayo na hudhani wamepoteza muunganiko na jamii yao hivyo hudhani dawa ni kujiua.
(ii) Altruistic suicide: Hili ni kundi la watu ambao hujiua kutokana na mshikamano uliopo katika jamii. Mapenzi na uzalendo wa hali ya juu katika jamii inayowazunguka hufanya baadhi ya watu kujiua kishujaa. Mathalani wanajeshi wanaweza kuona hatari mbele yao lakini wakawa mstari wa mbele kufa kwa ajili ya watu wao. Jamii inapokuwa imejengwa kwa mshikamano wa hali ya juu huwafanya baadhi ya watu kufa kwa ajili ya wengine, mfano mzuri ni wanajeshi.
(iii) Egoistic suicide: Watu wa kawaida wameunganishwa na jamii zao kwa sababu ama ya kazi wanazofanya, kwa sababu ya uhusiano kati ya jamii na jamii au muungano wa aina yoyote katika jamii. Inapotokea muunganiko huu ukapoteza nguvu au usiwepo tena kwa sababu mbalimbali ikiwa pamoja na kustaafu kazini au kupoteza familia au ndugu hufanya baadhi ya watu kujiua kwa sababu muungano wa kijamii uliokuwepo unakuwa haupo tena. Katika kundi hili, wazee wanaongoza kujiua.
(iv) Fatalistic suicide: Vifo vingi vya watu kujiua hapa husababishwa na sheria kali na kandamizi ambazo watu hudhani zinawanyima haki zao za kibinadamu. Katika hali kama hiyo watu huchagua kujiua kuliko kuishi katika ukandamizaji, mfano mzuri ni wafungwa gerezani. gerezani.
Ukiachana na mtaalamu huyo wa sosholojia, kwa ujumla mpaka kujinyonga au kujiua, huwa kuna hatua ambazo mtu anazipitia, lakini hatua ya mwisho kabisa ni mtu kuona amekataliwa hapa duniani, na jambo hilo humfanya kukata tamaa huku akiona watu wengine hawana msaada kwake. Msisitizo unabaki kuwa sababu za msingi za mtu kujiua ni za kijamii na si mtu binafsi.
Lakini mpaka mtu afikie hatua hiyo kubwa ya kudhani ‘amekataliwa’ huwa inatokana na msongo wa mawazo au mkandamizo wa mawazo, mfadhaiko au kudhoofishwa na matukio yaliyomtokea.
Matukio hayo nayo huwa yamesababishwa na mambo mengine ambayo yamemzunguka mtu katika jamii yake, lakini kwa kifupi sababu zote hizi husababisha mhusika kujikuta anafika hatua ya kuona ‘watu na dunia kwa ujumla wamemtenga’ na hivyo kuamua kujiua.
Kwa sababu polisi nao ni binadamu, nao huwa wanapita katika hatua hizi, lakini wao wanaweza kuwa na sababu za nyongeza zaidi tofauti na watu wa kazi nyingine.
Polisi wamefundishwa kuwa na siri na hivyo hata kama wana matatizo makubwa hujikuta wakishindwa kumwambia mtu yeyote siri zao, na mkusanyiko wa hayo husababisha wajione ‘dunia imewatanga’ na hudhani kujiua ndiyo msaada pekee.
Katika jambo la kushangaza Durkheim anasema kama idadi ya askari na raia ingekuwa inalingana, tungeshuhudia askari wengi wakijiua kuliko raia wa kawaida na hasa katika kipindi ambacho kuna amani. Anasema wakati wa vita kiwango cha askari kujiua hupungua kwa sababu wanakuwa na mshikamano zaidi.
Kwa ujumla jamii huwa na mshikamano zaidi wakati wa vita hivyo hata kiwango cha watu kujiua huwa kinapungua tofauti na wakati kukiwa na amani.
Durkheim anasema sehemu za kazi ambazo mifumo ipo imara, kiwango cha kujiua huwa ni kidogo tofauti na sehemu za kazi ambazo mifumo imeanza kulegea.
Polisi ambao huwa na ratiba inayofanana miaka nenda rudi; maisha yaleyale ya lindo, kaunta ya polisi, kuchukua maelezo na kwenda mahakamani huwa inafika mahali polisi anachoka na maisha hayo. Akichoka huona kama amejitenga na jamii inayomzunguka, kwa hiyo anapopata tatizo dogo tu kama wivu wa mapenzi au ugomvi huwa anachukulia kama tatizo kubwa na kujiua, ingawa hizo huwa si sababu ila ni vichocheo tu.
Kwa ujumla mpaka mtu anapofikia kuchukua uhai wake, anakuwa katika hali ya mwisho kabisa ya kuomba msaada, hata anapojinyonga huwa ni kuomba msaada, na si vinginevyo.
Jamii ina mchango mkubwa katika maisha ya mtu, kama mifumo ikiwa imara, taasisi zikawa imara, tamaduni zikabaki kuwa imara, tutashuhudia vifo vya aina hii vikipungua.

No comments

Powered by Blogger.