Full-Width Version (true/false)


Hii kali! Fei Toto asubuhi ametambulishwa Singida United, jioni ametambulishwa Yanga
Ndani ya saa 12, mchezaji wa JKU, Feisal Salum Abdalah “FEI TOTO” amesaini mkataba wa miaka mitatu asubuhi Singida United, ghafla Yanga imepindua meza kwa kumsainisha mchezaji huyo mkataba wa miaka mitatu jioni hii katika ofisi zao zilizopo mitaa ya Jangwani.
Mapema leo asubuhi Singida United ilitoa picha cha Fei Toto akiwa anasaini mkataba wa miaka miaka mitatu na klabu hiyo pamoja na kuvalishwa jezi.
Hata hivyo leo mchana mabingwa wa kihistoria, Yanga nao walitoa video za picha za Fei Toto akiwa na viongozi wa JKU pamoja na wale wa Yanga.
Yanga ni kama wameipiga bao Singida United kwani walianza kutoa picha zikimuonyesha mchezaji huyo anasaini akiwa na Mkurugenzi wa Singida United, Festus Sanga.
Kupitia kwa Meneja wa mchezaji huyo, Mohammed Kombo, alisema Singida hawakufata utaratibu na badala yake walikiuka taratibu zinazohitajika katika usajili.
"Feisal mpaka jioni saa kumi na nusu alikuwa bado mchezaji wa JKU, lakini kuanzia sasa ni mchezaji halali wa Yanga baada ya wao kumalizana na sisi," alisema Kombo.
Naye Feisal alisema yeye ni mali ya Yanga na  anatarajia kufanya mazuri akiwa na kikosi hiko.
"Mimi sina maneno mengi sana kikubwa natarajia kufanya makubwa nikiwa na Yanga na hivi sasa ni mchezaji halali wa Yanga," alisema kwa kifupi.
Wakati huo huo kiungo Jaffar Mohammed ambaye naye amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Yanga, alisema kwamba anatarajia kufanya vizuri kama ambavyo alivyokuwa akifanya katika timu zake za nyuma.
Huu ni usajili wa tatu kwa Yanga baada ya juzi kumsainisha kiungo Mohammed Issa 'Banka'.


No comments

Powered by Blogger.