Full-Width Version (true/false)


Hivi ndivyo Irene Uwoya anavyowaangusha wazazi wake


Irene Pancras Uwoya

MARA nyingi huwa tunaambiwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Kwa tafsiri nyingine isiyo rasmi ni kwamba, jinsi ulivyo ndivyo mtoto wako anavyoweza kuja kuwa.

Yani kama wewe ni mcha Mungu basi kuna uwezekano wanao nao wakawa wacha Mungu. Kama wewe ni mhuni basi hata ukijaaliwa watoto, nao wanaweza kuja kuwa wahuni. Tena wanaweza kuwa wahuni zaidi yako mpaka wewe mwenyewe ukashangaa.

Waswahili wanakwambia tabia ni kama ngozi huwezi kuibadili. Ukiwa mweupe wewe utakuwa mweupe tu, ukiwa mweusi vivyohivyo, huwezi kubadili labda utumie mkorogo ambao kimsingi unaondoa uhalisia wa jinsi Mungu alivyokuumba.

Kwenye ulimwengu wa mastaa, wapo ambao wanaishi maisha ambayo yanashabihiana na chimbuko la wazazi wao. Ukimuona muigizaji kama Jimmy Mafufu (wa sasa), utagundua kabisa ni kijana ambaye ametokea kwenye ukoo wa wachungaji.

Ukimuona msanii kama Ruth Suka ‘Mainda’ (wa sasa) maisha yake yanaakisi maadili mema. Ni mtu anayetambua hofu ya Mungu, anaishi kwa kufuata misingi ya dini inavyopaswa kuwa. Sawa na Jacob Stephen ‘JB’, pamoja na kuwepo kwa ‘mishale’ kadhaa inayompiga yeye lakini ukimtazama kwa makini utagundua ni mtu mwenye hofu ya Mungu.

Muigizaji Irene Pancras Uwoya ni miongoni mwa mabinti ambao kimsingi naweza kusema ametoka kwenye familia yenye maadili. Nionavyo mimi, mama na baba Uwoya ni wazee ambao wana hofu ya Mungu, wana maadili mazuri na wamewalea watoto wao katika misingi imara.

Ni wazee ambao wanatamani Uwoya kila siku aishi katika maadili mema, wanatamani kumuona akifanya sanaa kama kazi lakini si kazi kufanya mambo yasiyokuwa na maadili kwani kwa kufanya hivyo, itakuwa ni aibu kwao kama familia.

Uwoya baada ya kulelewa vyema na wazazi wake, mwaka 2006 walimruhusu ashiriki Shindano la Miss Tanzania. Yawezekana kulikuwa na ugumu ulikuwepo kutokana na jinsi mashindano hayo yalivyokuwa yakitafsiriwa vibaya na baadhi ya watu. Kuna watu walikuwa wanaona mashindano ya urembo ni kama uhuni. Lakini jitihada za kutoa elimu zilifanyika na hata baadhi ya wazazi ambao walikuwa wazito kuwaruhusu watoto wao washiriki hatimaye walikubali.

Umaarufu wa Uwoya ulishamiri mara baada ya kushiriki na kuwepo ndani ya Tano Bora. Baada ya hapo akatupa karata yake kwenye upande wa filamu, maisha ya umaarufu yakaanzia hapo. Alionesha uwezo mkubwa katika filamu, alionesha anajua nini anatakiwa kufanya anapokuwa mbele ya kamera.

Uzuri wa umbo lake ndio uliomkosha hata marehemu mumewe, Hamad Ndikumana ambaye alimuona kupitia Filamu ya Oprah akampenda na kuamua kuomba urafiki, uchumba na baadaye ndoa takatifu katika Kanisa la Mt. Joseph, Posta Dar es Salaam.

Hili lilikuwa pia ni tendo takatifu ambalo linaakisi misingi mizuri ya wazazi ambao wamemlea mtoto katika maadili. Wapo warembo wengi wenye mvuto wa kila aina lakini hawaolewi Wanatangatanga tu na dunia kutokana na misingi mibaya waliyowekewa na wazazi wao au kujiwekea wao wenyewe.

Kwa mantiki hiyo, ndoa ya Uwoya ilikuwa na baraka zote za wazazi wake. Akaingia kwenye ndoa na maisha yao yalikuwa mazuri, wakajaaliwa kupata mtoto mmoja (Krish) na marehemu mumewe. Lakini kuna kitu Uwoya anapaswa kujua kwamba, staili anayokwenda nayo kwa sasa haifanani sana na misingi ya wazazi wake.

Haya mapicha ya nusu utupu anayoachia mtandaoni, hayafanani sana na misingi ya wazazi wake. Hii inaonesha dhahiri kwamba hata wazazi wake watakuwa hawafurahishwi na matukio ya namna ile. Kitendo cha kufunga ndoa na Dogo Janja bila uwepo wa wazazi wake ni tatizo.

Mama kutamka hadharani kwamba hamtambui Dogo Janja ni ishara mbaya ya mwenendo wa Uwoya. Anawaangusha wazazi wake ambao walitamani wamuone kwenye maadili mazuri. Wanatamani kumuona anafanya mambo yanayofanana na wao walivyo. Uwoya ana kila sababu ya kujisahihisha, kuwatazama wazazi wake walikomtoa na hapa alipo sasa. Anaweza kujisahihisha na kurudi kwenye misingi mizuri ambayo hata wazazi wake watajivunia maisha yake!

No comments

Powered by Blogger.