Full-Width Version (true/false)


Hofu yatanda kwa Wananchi baada ya Mwanamke kuchinjwa Tanga


KAMANDA WA POLISI MKOA WA TANGA, EDWARD BUKOMBE.
MAUAJI ya mkazi wa Mtaa wa Japan Kata ya Tangasisi Wilaya ya Tanga, Hidaya Shaban (34), yamezusha hofu kwa wananchi wa Jiji la Tanga kutokana na aina ya kifo chake kuwatokea watu zaidi ya watatu kwa kipindi kifupi.


Mauaji hayo ambayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, ni ya mwanamke mfanyabiashara ambaye mwili wake uliokotwa eneo la mtaa wa Japan Kata ya Tangasisi.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Bukombe alieleza kuwa lilitokea Jumamosi usiku na kwamba marehemu alikuwa mfanyabiashara ambaye kifo chake kilitokana na kuchinjwa kama mnyama.Kwa mujibu wa kamanda huyo, polisi inaendelea na uchunguzi wa mauaji hayo ambapo msako mkali unaendelea kwenye mitaa ya Jiji la Tanga.


“Marehemu alikutwa ameburuzwa umbali wa mita 500 kutoka sehemu alipouawa... mwili wake haukukutwa na nguo za ndani, jambo linalolifanya Jeshi la Polisi kuingia wasiwasi kwamba huenda alifanyiwa kitendo cha udhalilishaji wa kijinsia kabla ya kuuawa,” alisema Bukombe.Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wakazi wa Jiji la Tanga walielezea hofu yao kwa kile walichodai kuwa ni mauaji yanayofanana na kwamba mara zote wauaji hao hawachukui kitu chochote cha marehemu.“Suala hili tunataka polisi waeleze ukweli nani muuaji kwa kuwa ni mara ya nne sasa watu wanaokotwa wakiwa wameuawa kinyama bila wauaji hao kuchukua chochote...inatia shaka,” alieleza Mashaka Rajab, mkazi wa Mtaa wa Japan.
 


Kwa upande wao,  mmoja wa wakazi  wa nyumba aliyokuwa akiishi marehemu Hidaya, alisema kuwa Jumamosi jioni Hidaya aliwaaga kwamba anakwenda kulipa madeni aliyokuwa akidaiwa, lakini hakuweza kurejea tena hadi walipopata taarifa kuwa kuna mwiliumeonekana karibu na shule ya Sekondari Japan na kubainika ni yeye.Akieleza bila kutaka kuandikwa jina gazetini, shuhuda huyo alisema tukio hilo liliwashtua kwa sababu ni kawaida kwa mfanyabiashara huyo kuaga kwamba anakwenda kulipa madeni na kurejea nyumbani mapema.David John, mkazi wa Mwang’ombe, alieleza kushangazwa kwake namna ya matukio ya mauaji hayo yanavyofanana na kudai kuwa mauaji kama hayo yameshafanyika zaidi ya mara tatu kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.


“Inavyoonekana mauaji hayo yanapangwa na watu ama kikundi maalum…kwa nini watu wanachinjwa na mali zao kuwa salama,” alisema na kuendelea: “kwanini Jeshi la Polisi lisitoe taarifa za mauaji haya. Yanatisha, watu wanahofu.”


Wakati wananchi wakieleza hofu yao, Kamanda Bukombe aliwataka wasiwe na hofu kwa kusema kuwa mauaji hayo ni ya kawaida na kwamba watahakikisha wahalifu hao wanadhibitiwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

No comments

Powered by Blogger.