Full-Width Version (true/false)


Kocha Croatia azitosa klabu za England kimtindo

 

Moscow, Russia. Kuelekea mechi ya fainali ya Kombe la Dunia kati ya Ufaransa na Croatia, Kocha wa Croatia, Zlatko Dalic ameamua kupuuza tetesi zinazomhusisha kutakiwa na klabu za Ligi Kuu England, akisisitiza akili yake ni mechi ya leo na sio vinginevyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, kocha huyo aliyechukua jukumu la kukinoa kikosi cha watoto wa Mama kutoka kwa Ante Cacic, siku chache kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia na kufanikiwa kuushangaza ulimwengu kwa kuifikisha Croatia fainali.

"Siwezi kufikiria kitu kingine zaidi ya Kombe la Dunia. Kila kitu na wakati wake. Kwa sasa tunawaza mechi ya kesho, nimesikia kuna klabu zinanitaka lakini sidhani kama kuna haja ya kuliwazia hilo kwa sasa. Labda baada ya Kombe la Dunia," alisema Dalic.

Kuna tetesi kuwa Chelsea walikuwa wanafikiria kumchukua Kocha huyo kabla ya nafasi hiyo kukabidhiwa kwa Kocha wa Napoli Maurizio Sarri ambaye anachukua mikoba ya Antonio Conte aliyetupiwa virago baada ya kushindwa kuipa Chelsea mafanikio waliyoyataka msimu uliopita.

Croatia na Ufaransa zinakutana katika mechi ya fainali, kusaka bingwa wa makala ya 21 ya Kombe la Dunia, ambayo yamekuwa yakitimua vumbi katika ardhi ya Warusi, kuanzia Juni 14.  Mechi hiyo itafanyika katika dimba la Luzhniki, kuanzia saa 12 jioni na kuchezeshwa na Muargentina Nestor Pitana.

No comments

Powered by Blogger.