Full-Width Version (true/false)


Kocha Yanga ajinadi Angola

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Yanga, Mserbia, Kostadin Papic, ametua Angola kwa ajili ya kusaka ajira ya kuinoa timu ya Taifa ya nchi hiyo, imefahamika. 

Akizungumza na gazeti hili jana, Papic alisema yuko nchini humo kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo ambayo waliyaanza na viongozi wa soka wa nchini humo akiwa kwao Serbia. 

Papic alisema wako makocha wengi ambao wameomba ajira ya kuifundisha Angola na kikao cha kuamua nani atapewa ajira hiyo kinatarajiwa kujulikana mapema Septemba mwaka huu. Kocha huyo aliongeza kuwa kwa sasa anaamini ana uwezo wa kufundisha timu ya taifa yoyote baada ya kufanya vizuri akiwa na klabu mbalimbali barani Afrika. 

"Kwa sasa niko Angola, nimekuja kuendelea na mazungumzo kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuifundisha timu yao ya Taifa, hilo ndio lengo langu kwa sasa, ila wamesema watakamilisha mchakato Agosti 31 na Septemba tutafahamu walichoamua mabosi wa soka wa nchi hii," alisema Papic. 

Mserbia huyo pia alianza mawasiliano na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba baada ya kusikia Mfaransa, Pierre Lechantre, ameondoka na vile vile aliitamani Azam FC ambayo tayari imeingia mkataba na Mholanzi, Hans van der Pluijm. 

"Yanga hapana, nasikia wana matatizo ya fedha, ni ngumu kufanya kazi katika hali hiyo, kama kurudi kwa mara nyingine Tanzania, iwe ni kufundisha Simba au Azam FC," Papic aliongeza. 

Mwaka 2012 wakati Simba wanaifunga Yanga mabao 5-0, Papic alikuwa jukwaani na hiyo ilitokana na kutofautiana na viongozi waliokuwa madarakani, hivyo hakuwa sehemu ya benchi la ufundi.

No comments

Powered by Blogger.