Full-Width Version (true/false)


Kodi za mtandao zazua kizaazaa UgandaPOLISI nchini hapa imefikia hatua ya kufyatua risasi zinazotoa machozi hewani, kutawanya kundi la waandamanaji wanaopinga kodi iliyoidhinishwa ya kutumia mitandao ya kijamii.

Ni maandamano yanayodaiwa kuhamasishwa na mbunge, Robert Kyagulany, ambaye ni mwimbaji mashuhuri anayefahamika kwa jina la ‘Bobi Wine’, aliyeongoza maandamano hayo, lakini amefanikiwa kutoroka.

Kodi hiyo iliyoidhinishwa mwanzoni mwa mwezi huu, inawataka watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini, kulipa fedha Shilingi 200 za Uganda( Dola za Marekani 0.05 au Pauni ya Uingereza 0.04) ambayo ni sawa na Shilingi 142,  ili waweze kutumia mitandao kama Facebook, Twitter na WhatsApp. Bunge liliidhinisha kodi hiyo Mei mwaka huu na zimaeanza kutumika mwezi huu.

Katika barua aliyomwandikia Waziri wa Fedha mnamo Machi mwaka huu, Rais Yoweri Museveni, alisema kodi kwa mitandao ya kijamii inaweza kuongeza kipato serikali na kupunguza mikopo inayochukuliwa na serikali, pia pesa za wafadhili.

Anasema, haungi mkono kodi kutozwa kwa matumizi ya jumla ya mtandao, kwa sababu itaathiri matumizi yake kwa misingi ya 'elimu na utafiti '.

Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Uganda, Frank Tumwebaze pia ametetea kuidhinishwa kwa kodi hiyo, akisema fedha zitakazopatikana zitatumiwa kuwekeza katika rasilimali zaidi za kimitandao.

Baadhi ya watu wanalalamika kuwa, hiyo ni njia ya kubana au kuzuia kauli zinazoikosoa serikali. Inakadiriwa kwamba zaidi ya asilimia 70 ya raia nchini Uganda wana simu za mkononi.

Pia, inakadiriwa kuwa asilimia 41 ya raia wa Uganda wanatumia mtandao na kuifikia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter, ambayo ni maarufu katika sehemu nyingi duniani, kwa mujibu wa utafiti wa kitaifa wa Mamlaka ya Habari na Teknolojia Uganda (NITA-U).

Mataifa mengine ya Afrika Mashariki, nayo yamechukua hatua ya kudhibiti matumizi ya mitandao, ambayo wakosoaji wanasema zinaathiri uhuru wa watu kujieleza.

Watumiaji mitandao ya kijamii nchini Uganda,   wanaelezwa katika hali halisi hawana namna ya kukwepa tozo hilo la kodi ya mitandao ya kijamii iliyoidhinishwa na serikali.

Pia, kuna agizo lililotolewa kwa kampuni za mawasiliano za Uganda, kuzuia mfumo unaoruhusu watumiaji mitandao kuweza kupitiliza baadhi ya mipaka, kwani inadaiwa hali iliyoko sasa, wateja wanavuka vizuizi vilivyowekwa kuwaruhusu kuingia katika mitandao hiyo ya kijamii na kukwepa kulipa Kodi.

Kwa mujibu wa serikali ya Uganda, serikali sasa inasema hilo linaelekea kufikia ukomo. Wananchi hawatakwepa malipo ya kodi za mtandao.

Serikali inasema, hatua hiyo itasaidia kuingiza kipato kinachohitajika pakubwa, lakini wanaharakati wanaikosoa hatua hiyo kuwa ya jaribio la 'kubana' uhuru wa kuzungumza.

Gazeti moja liliripoti kwamba, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Mawasiliano Uganda, Godfrey Mutabazi, akisema kampuni za simu zitaanza kuzuia programu zinazowasaidia Waganda kukwepa kulipa kodi ya mitandao ya kijamii.

Ni kwanini kodi?
Rais Museveni alishinikiza mageuzi hayo, akieleza kuwa mitandao ya kijamii huchangia kuenea kwa udaku nchini, anaoutaja kuwa maoni, upendeleo, matusi na hata kuchati kwa marafiki.

Katika barua aliyomwandikia Waziri wa Fedha mnamo Machi, Rais Museveni amesema kodi kwa mitandao ya kijamii inaweza kuongeza kipato cha serikali, na kupunguza mikopo inayochukua serikali na pesa za ufadhili.

Aliongeza kwamba haungi mkono kodi iitozwe kwa matumizi ya jumla ya mtandao kwa sababu hili litaathiri matumizi yake kwa misingi ya 'elimu, na utafiti '.

Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Uganda, Frank Tumwebaze, alitetea kuidhinishwa kwa kodi hiyo, akisema kwamba fedha zitakazopatikana zitatumiwa ‘kuwekeza katika rasilimali zaidi za kimitandao.”

Agizo hilo la kulipa kodi kwa mitandao kama Whatsapp, Facebook, Twitter limeanza kufanya kazi tarahe moja mwezi huu.

Agizo limepokewaje? Kumeibuka hisia mchanganyiko miongoni mwa raia wa Uganda, wengi wakieleza walivyoathirika nalo, huku wengine wakilipa kodi hiyo. BBC

No comments

Powered by Blogger.