Full-Width Version (true/false)


Kuingia Mirerani sasa kwa vitambulisho vya Taifa

 

Baada ya Tume ya Madini iliyoundwa na Rais John Magufuli kubaini utoroshwaji wa madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Manyara imezuia magari kuingia ndani ya ukuta huo unaozunguka migodi ya madini hayo.
Jana gazeti hili la Mwananchi lilimnukuu mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Idris Kikula akisema kuwa utoroshaji wa madini hayo ya vito umesababisha mrabaha kushuka kutoka Sh444 milioni hadi Sh40 milioni kwa mwezi.
Hadi kufikia saa 7:00 mchana jana, magari yaliyokuwa yamebeba maji pamoja na yaliyobeba wachimbaji na wanunuzi yali zuiwa kuingia migodini.
Pia, wachimbaji wadogo walizuiwa kutumia lango hilo kuingia migodini, wakitakiwa kuonyesha vitambulisha vya Taifa na vile vinavyotolewa na Wizara ya Madini, hali iliyoibua mtafaruku kutokana na wengi kutokuwa navyo.

Kwa siku nzima ya Jumatano, kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na mkuu wa mkoa huo, Alexander Mnyeti, kamanda wa polisi, Agostino Senga na mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula, ilikuwa eneo la mgodi kufanya kikao.
Mmoja kati ya wamiliki wa migodi ya Tanzanite, Abubakary Mwamba alisema wachimbaji wadogo wamekwamishwa kufanya kazi yao kutokana na masharti hayo ya kutakiwa kutotumia magari kuingia na kuonyesha vitambulisho hivyo.
"Magari yameshindwa kupita kwenye lango kutokana na utaratibu huo mpya wa upekuaji. Tumeambiwa kuwa wizara imeagiza hali hii," alisema Mwamba.
Alisema Serikali inapaswa kujipanga kwanza ili kufanikisha zoezi hilo kuliko kuanza kutaka vitambulisho vitumike ilihali bado hawajajiandaa vya kutosha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini wa Manyara (Marema), Sadiki Mneney alisema hawapingi hatua ya Serikali kufuatilia mapato kupitia migodi hiyo, ila utaratibu unapaswa kuwekwa vizuri.
"Wachimbaji wengi hawana hivyo vitambulisho vya Taifa na vilivyotolewa na wizara na vitambulisho vya mpigakura havitakiwi kutumiwa," alisema Mneney.
Alisema wachimbaji hawapingi zoezi hilo kwa kuwa lina manufaa kwa Taifa katika kufuatilia mapato, lakini akaitaka iweke utaratibu vizuri.
Hata hivyo, bado vifaa vya ukaguzi, upekuzi na taa zilizoahidiwa kuwekwa na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa ukuta huo, bado hazijawekwa.
Hivi sasa, askari polis,i maofisa madini na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ndiyo wanalinda lango kuu kwa kuhakikisha wanawatambua wanaoingia na wanaotoka migodini.


No comments

Powered by Blogger.